Larijani: Litaundwa kundi la kuchunguza shambulio la kemikali huko Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i27502-larijani_litaundwa_kundi_la_kuchunguza_shambulio_la_kemikali_huko_syria
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran yaani Bunge amelaani mashambulizi ya makombora ya Marekani huko Syria kwa kisingizio cha kutekelezwa shambulio la kemikali nchini humo na kutaka kuundwa kundi la kuchunguza suala hilo.
(last modified 2026-02-15T09:07:51+00:00 )
Apr 09, 2017 07:03 UTC
  • Larijani: Litaundwa kundi la kuchunguza shambulio la kemikali huko Syria

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran yaani Bunge amelaani mashambulizi ya makombora ya Marekani huko Syria kwa kisingizio cha kutekelezwa shambulio la kemikali nchini humo na kutaka kuundwa kundi la kuchunguza suala hilo.

Ijumaa ya juzi tarehe Saba Aprili Marekani ilikishambulia kwa makombora ya cruz kituo cha jeshi la anga la Syria huko al Shayrat kwa kisingizio kwamba, jeshi la Syria lilitumia silaha za kemikali kufanya mashambulizi latika eneo la Khan Sheikhoun katika mji wa Idlib kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. 

Akizungumza katika kikao cha wazi cha bunge hii leo, Ali Larijani Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amekosoa mashambulizi ya Marekani katika kituo cha anga cha Syria na kuongeza kuwa: Serikali ya Marekani imetegemea kisingizio cha kutumiwa silaha za kemikali na kuamua kuishambulia Syria na kuisababishia maafa nchi hiyo bila ya kuthibitisha madai yake wala kufanywa uchunguzi na taasisi za kimataifa.

Maafa ya mashambulizi ya Marekani katika kituo cha anga cha Syria  

Spika wa bunge la Iran ameashiria kimya cha Marekani na serikali nyingine za Magharibi mkabala na mashambulizi ya kemikali yaliyotekelezwa na utawala wa Baath wa Iraq katika vita vya miaka minane vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran na kueleza kuwa, Iran inapinga mshambulizi yoyote ya kemikali na vilevile kulaani kutolewa madai ya uwongo katika uwanja huo yanayopelekea kuchukuliwa hatua za kichokozi.