Zarif atoa wito wa kupambana na ugaidi na misimamo ya kuchupa mipaka
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28312-zarif_atoa_wito_wa_kupambana_na_ugaidi_na_misimamo_ya_kuchupa_mipaka
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema jitihada za pamoja za kimataifa zinahitajika ili kung'oa mizizi ya ugaidi na kuenea wimbi la misimamo mikali ya kufurutu ada.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 27, 2017 03:24 UTC
  • Zarif atoa wito wa kupambana na ugaidi na misimamo ya kuchupa mipaka

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema jitihada za pamoja za kimataifa zinahitajika ili kung'oa mizizi ya ugaidi na kuenea wimbi la misimamo mikali ya kufurutu ada.

Zarif aliyasema hayo jana katika mkutano wake na Chynybai Tursunbekov, Spika wa Bunge la Kyrgyzstan ambaye yuko safarini hapa nchini na kuongeza kuwa, ugaidi ni tishio sio tu kwa nchi za eneo hilo bali kwa nchi zote za dunia.

Dakta Zarif amesisitiza kuwa, kuna haja jamii ya kimataifa iimarishe uhusiano na ushirikiano wa nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kupambana na jinamizi la ugaidi akifafanua kwamba, jukumu hilo sio la dola au serikali moja tu.

Kwa upande wake, Chynybai Tursunbekov, Spika wa Bunge la Kyrgyzstan ameashiria juu ya uhusiano mzuri wa kiutamaduni na kihistoria kati ya nchi mbili hizi, ambao unarejea nyuma zaidi ya miaka elfu 5 na kufafanua kuwa, ushirikiano huo umekuwa na nafasi chanya kieneo na kimataifa.

Maspika wa Mabunge ya Iran na Kyrgyzstan

Amebainisha kuwa, moja ya matunda ya uhusiano huo ni makubaliano ya kihistoria ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 yanayofahamika kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Spika wa Bunge Kyrgyzstan amesema kipindi hiki nyeti cha utekelezwaji wa makubaliano hayo ni fursa ya kipekee ya kumarisha uhusiano wa pande mbili kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu, huku akitumai kuwa, wawekezaji wengi wa Kiirani watafurika kwenye masoko ya nchi yake.