Iran: Marekani, Israel na Uingereza haziutakii kheri umma wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28432-iran_marekani_israel_na_uingereza_haziutakii_kheri_umma_wa_kiislamu
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kuwepo kijeshi Marekani na nchi za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati kuna madhara makubwa kwa mataifa ya eneo hili kwani licha ya kuja na kaulimbiu ya kuimarisha usalama na amani, lakini madola hayo ya kibeberu ndiyo sababu kuu ya kutoweka amani na usalama katika eneo hili.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 30, 2017 02:33 UTC
  • Iran: Marekani, Israel na Uingereza haziutakii kheri umma wa Kiislamu

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kuwepo kijeshi Marekani na nchi za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati kuna madhara makubwa kwa mataifa ya eneo hili kwani licha ya kuja na kaulimbiu ya kuimarisha usalama na amani, lakini madola hayo ya kibeberu ndiyo sababu kuu ya kutoweka amani na usalama katika eneo hili.

Brigedia Jenerali Hussein Dehqan amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya "Russia al Yaum" na huku akigusia tofauti zilizopo baina ya Iran na nchi za Magharibi kuhusu maana ya neno ugaidi amesema: Kwa mtazamo wa Magharibi, gaidi ni mtu ambaye anahatarisha malengo ya kimataifa ya mabeberu katika eneo lolote lile duniani, lakini Iran haikubaliani na maana hiyo bali inaamini kuwa, mataifa na watu wote duniani wana haki ya kusimama kidete kupigania haki zao, na wanapofanya hivyo kamwe hawawezi kuitwa magaidi.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani akiwa ziarani nchini Saudi Arabia ambayo inatumia fedha nyingi za wananchi kuomba ulinzi na uungaji mkono wa madola ya Magharibi hasa Marekani

 

Waziri wa Ulinzi wa Iran amezilaumu nchi za Magharibi kwa kuendesha siasa za nyuso mbili kuhusiana na ugaidi na kusema kwa kusisitiza kwamba: Si sahihi hata kidogo kuugawa ugaidi baina ya mzuri na mbaya, kama ambavyo pia haikubaliki kuyaangalia matukio ya dunia kwa kioo cha Marekani na baadaye kusema tukio hili ni ugaidi na hili si ugaidi.

Aidha amesema, Iran haiingilii masuala ya ndani ya majirani zake lakini inasikitisha kuona kuwa leo hii Saudi Arabia imekuwa wakala wa Marekani na Israel katika eneo hili kiasi kwamba hata fedha za nchi za Kiarabu kama vile Saudi Arabia zinatumika hivi sasa kulinda usalama wa Israel.

Vile vile amezionya pande nyingine zilizofikia makubaliano ya nyuklia na Iran kama vile Marekani kwamba iwapo zitavunja makubliano hayo, Iran nayo itayavunja na haitakubali kuwa nchi pekee inayoheshimu makubaliano hayo.