Iran: Kauli ya Salman ni ithibati kuwa Saudia inaunga mkono ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i28620-iran_kauli_ya_salman_ni_ithibati_kuwa_saudia_inaunga_mkono_ugaidi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Naibu Mrithi wa Kiti cha Ufalme ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia ni dhihirisho tosha kuwa Riyadh inaunga mkono ugaidi na utawala huo wa kifalme umejengeka katika misingi ya sera haribifu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 03, 2017 23:33 UTC
  • Iran: Kauli ya Salman ni ithibati kuwa Saudia inaunga mkono ugaidi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Naibu Mrithi wa Kiti cha Ufalme ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia ni dhihirisho tosha kuwa Riyadh inaunga mkono ugaidi na utawala huo wa kifalme umejengeka katika misingi ya sera haribifu.

Hayo yamesemwa na Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ambaye amefafanua kuwa, matamshi hayo ya chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Mohammad Bin Salman Al Saud, kwa mara nyingine tena yameuonyesha ulimwengu kuwa utawala wa Aal-Saud unaendelea kufuata sera zake haribifu na za uhasama ambazo zimekuwa na taathira hasi kwa eneo lote la Mashariki ya Kati.

Katika mahojiano na kanali ya televishani ya al-Arabiyyah ya nchi hiyo siku chache zilizopita, Bin Salman alibainisha chuki yake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kusema wazi kwamba, Saudia katu haitakuwa na mahusiano mazuri na Tehran.

Salman (kulia) na Rais wa Marekani Donald Trump

Kuhusu mgogoro wa Yemen, Waziri wa Ulinzi wa Saudia alitoa madai ya kuchekesha kwamba, harakati ya kujitolea ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah ni hatari kimataifa na kwa nchi za eneo la Mashariki ya Kati na kuwa eti Riyadh iliingia katika vita dhidi ya Yemen kwa ajili ya kuzilinda nchi za eneo la Mashariki ya Kati. Hii ni licha ya ukweli kwamba, hujuma za Saudia dhidi ya Yemen hadi sasa zimesababisha zaidi ya watu elfu 12 kuuawa, makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi tangu Machi 2015.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, Tehran daima imekuwa ikifadhilisha kupatiwa ufumbuzi migogoro na changamoto zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu kwa njia za kuimarisha uhusiano na ushirikiano lakini mizozo hiyo imekuwa ikipata nguvu kutokana na sera za chuki na uhasama za utawala wa Aal-Saud, unaounga mkono ugaidi kwa kutumia idiolojia ya Uwahabi.