Zarif: Ukurasa mpya umefunguliwa katika uhusiano wa Iran na Australia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Javad Zarif amesema ukurasa mpya umefunguliwa katika uhusiano wa Iran na Australia.
Zarif ameyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Julie Isabel Bishop huko mjini Canberra. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Iran na Australia zina uhusiano wa kihistoria, na hivi sasa yamejitokeza mazingira mapya kwa ajili ya uhusiano baina ya nchi mbili.
Amesema amefanya mazungumzo yenye taathira chanya na waziri mwenzake wa Australia na kuongeza kuwa ajenda za mazungumzo hayo zilihusu kustawishwa uhusiano baina ya nchi mbili katika sekta za biashara, uwekezaji, teknolojia na uchumi. Dakta Zarif amesema kupambana na vitendo vya ukatili na vya kufurutu mpaka pamoja na jinai zilizoratibiwa, ni ajenda nyengine zilizokuwemo katika mazungumzo hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa Uislamu ni dini ya amani na upendo na inapinga mielekeo ya kufurutu mpaka, hata hivyo hivi sasa Waislamu wamekuwa wahanga wa vitendo vya ukatili.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Bi Julie Isabel Bishop ameashiria kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran na kueleza kuwa hivi karibuni nchi yake iliondoa vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na iko tayari kustawisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na Iran.../