Khatibu: Makombora ya IRGC yalikuwa jibu muafaka kwa magaidi
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo mjini Tehran Ayatullah Imami Kashani amesema hatua ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, IRGC, kushambulia kwa makombora ngome za magaidi wa ISIS nchini Syria ilikuwa ni jibu muafaka na adhabu kwa magaidi hao wakufurishaji.
Tarehe 18 Juni, IRGC ilivurumisha makombora sita kuelekea katika ngome kadhaa za magaidi wa ISIS huko Deir Ezzor nchini Syria. Makombora hayo yaliyorushwa kutoka Iran yaliptia juu ya anga ya Iraq na kuenda masafa ya kilomita 650 na kulenga ngome za ISIS ndani ya ardhi ya Syria na kusababisha hasara na maafa makubwa kwa magaidi. Oparesheni hiyo ilikuwa ni ya kulipiza kisasi baada ya magaidi wa ISIS kutekeleza hujuma mbili za kigaidi mjini Tehran na kuwaua kidhalimu watu 18 katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Jeshi la IRGC lilitangaza kuwa halitaacha damu hiyo takasifu imwagike bila ya jibu na baada ya siku 12 makombora yakawalenga magaidi hao wa ISIS.
Katika hotuba yake, Ayatullah Imami Kashani amesisitiza kuwa, magaidi na waungaji mkono wao wafahamu kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa jibu kali kwa hujuma na uchokozi wowote dhidi yake. Aidha amesema usalama ulioko Iran ni wa aina yake na kusema uwezo mkubwa wa kijeshi na kisayansi wa Iran ni baraka za Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoongozwa na Imam Khomeini, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu.
Aidha Ayatullah Kashani pia ametoa pongezi kwa serikali na taifa la Iraq kufuatia kukombolewa mji wa Mosul uliokuwa unakaliwa na magaidi wa ISIS na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni na utawala wa Saudia ni waungaji mkono wakuu wa magaidi katika eneo.