Marekani yajaribu kupotosha dunia kuhusu inavyounga mkono ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i32028-marekani_yajaribu_kupotosha_dunia_kuhusu_inavyounga_mkono_ugaidi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Marekani imetoa ripoti kuhusu hali ya ugaidi duniani ili kwa njia hiyo ipotoshe fikra za waliowengi kuhusu nafasi yake katika kuibua, kueneza na kuunga mkono makundi ya kigaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2017 09:20 UTC
  • Marekani yajaribu kupotosha dunia kuhusu inavyounga mkono ugaidi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Marekani imetoa ripoti kuhusu hali ya ugaidi duniani ili kwa njia hiyo ipotoshe fikra za waliowengi kuhusu nafasi yake katika kuibua, kueneza na kuunga mkono makundi ya kigaidi.

Siku ya Jumatano, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa ripoti ya kila mwaka kuhusu hali ya ugaidi duniani na kwa mara nyingine kudai eti Iran inaunga mkono ugaidi.

Akitoa jibu kwa ripoti hiyo, msemaji wa  Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi  amesema ripoti hiyo inaashiria sera zilizojaa chuki na kutumiwa ugaidi kwa malengo ghalati kama ilivyokuwa katika miaka ya huko nyuma.

Qassemi ameongeza kuwa, ripoti hiyo ya Marekani imepuuza mtazamo wa waliowengi duniani kuwa Iran inakabiliana  na ugaidi hatari zaidi katika eneo. Amesema ripoti hiyo ya Marekani kuhusu ugaidi imetumia mbinu zisizozingatia ukweli wa mambo na hivyo kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran.

Qassemi amesema Marekani inaunga mkono baadhi ya nchi katika eneo ambazo ndizo kituo cha kifikra cha makundi makubwa zaidi ya kigaidi duniani na kusema: "Katika hali ambayo wakuu wa Marekani wenyewe, vyombo vya habari na Wamarekani waliowengi wanakiri kuhusika nchi hiyo (Saudi Arabia) katika hujuma nyingi za kigaidi, lakini Marekani imeichukua nchi hiyo kama muitifaki wake katika vita dhidi ya ugaidi."

Rais Trump akicheza densi ya kijahilia na mfalme wa Saudia, nchi ambayo ni chimbuko la fikra za ugaidi

Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kupabana na makundi ya  kigaidi na yenye misimamo maikali ambayo ni tishio kubwa zaidi kwa usalama duniani na kwamba tuhuma hizo zisizo na msingi hazitabadilisha azma ya nchi hii kukabiliana na magaidi.