Rais Hassan Rouhani: Iran itatoa jibu kali kwa Marekani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran itatoa jibu kali kwa hatua ya Marekani ya kupasishwa vikwazo vipya dhidi ya taifa hili.
Rais Hassan Rouhani amesisitiza kwamba, hatua ya Kongresi ya Marekani ya kupasisha vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu haitaachwa hivi hivi na Iran bali taifa hili litatoa jibu kali kwa hatua hiyo.
Tarehe 15 ya mwezi uliopita wa Juni, Seneti ya Marekani iliendeleza hatua za kihasama za nchi hiyo dhidi ya Iran na Russia kwa kupitisha mpango mpya wa vikwazo dhidi ya nchi hizo mbili, lakini upigiaji kura mswaada huo uliahirishwa katika Baraza la Wawakilishi la Marekani baada ya wajumbe wa chama cha Republican kutoa pendekezo la kujumuishwa Korea Kaskazini kwenye kifurushi hicho kipya cha vikwazo dhidi ya Tehran na Moscow. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Seneti walikubaliana kupitisha marekebisho ya mswada huo Jumanne ya jana.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Mawaziri, Rais Rouhani amesema kuwa, Marekani inapaswa kuheshimu haki za taifa la Iran na itambue kwamba, ni kwa kuheshimu haki za raia na kutanguliza mbele njia za amani ndipo maslahi ya wananchi wa Marekani yatakapodhaminiwa.
Amesema, Marekani haina uhasama na uadui na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu tu, bali hata haiko tayari kuona Iran ikisimama kidete na kuwa kigezo kwa mataifa mengine.