Larijani: Tume ya kutafuta ukweli ya UN ichunguze hali ya Myanmar
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amelaani mauaji ya Waislamu wa Myanmar na kutaka ujumbe wa kutafuta ukweli wa Umoja wa Mataifa utumwe haraka nchini humo kuchunguza hali ya mambo na utumaji misaada ya kibinadamu.
Ali Larijani ameeleza kusikitishwa na matukio ya kusononesha, mauaji, ukandamizaji na kuhamishwa kwa nguvu makumi ya maelfu ya Waislamu Warohingya nchini Myanmar na kusisitiza kwamba maafa hayo ni matokeo ya kimya cha wanaojidai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu na baadhi ya nchi na jumuiya za kimataifa ambazo zimebaki kuwa watazamaji tu wa matukio hayo ya kutisha, ukiukaji haki za binadamu na mauaji ya kimbari ya Waislamu nchini Myanmar.
Spika wa Bunge la Iran amesisitizia jukumu zililonalo nchi zote, mabunge, asasi na jumuiya za kieneo na kimataifa hususan Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya ushirikiano wa Kiislamu (OIC) la kuleta amani na utulivu katika eneo na kuwahami Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.
Zaidi ya Waislamu 400 Warohingya wa jimbo la Rakhine lililoko magharibi mwa Myanmar wameuawa katika mashambulio ya jeshi la nchi hiyo yaliyoanza tarehe 25 ya mwezi uliopita wa Agosti. Serikali ya Myanmar inawahesabu Waislamu wapatao milioni moja Warohingya kuwa ni wahajiri haramu na wala haiwapi haki zozote za kiraia.../