Zarif autaka Umoja wa Mataifa kusitisha mauaji ya Waislamu Myanmar
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kusitisha ukatili unaofanyika kwa mpangilio maalumu dhidi ya Waislamu nchini Myanmar.
Barua hiyo ya Muhammad Javad Zarif kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres imetahadharisha kuhusu ukatili unaoendelea kufanywa dhidi ya Waislamu wa Myanmar na kusema: Jamii ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa, inalazimika kuchukua hatua katika uwanja huo.
Tangu Ijumaa ya tarehe 25 Agosti Waislamu wasiopungua elfu 6 na 334 wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wameuwa na wengine 349 kujeruhiwa katika wimbi jipya la mashambulizi na ukandamizaji unaofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu katika mkoa wa Rakhine.
Waislamu wa eneo hilo la Rakhine wamekuwa wakishambuliwa na kuuawa na Mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na jeshi la Myanmar tangu mwaka 2010.
Waislamu milioni moja wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wananyimwa haki zao za kimsingi ikiwemo haki za uraia na maelfu miongoni mwao wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mauaji na ukatili unaofanywa na jeshi na Mabudha wa nchi hiyo.