Mpango wa kujitenga Kurdistan na Iraq ni njama za Wazayuni
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa Tehran amesema, kura ya maoni ya kujitenga na Iraq eneo la Kurdistan ni njama ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ayatullah Mohammad Imami Kashani aidha amesema katika hotuba zake za sala ya Ijumaa ya leo hapa mjini Tehran kwamba, iwapo eneo la Kurdistan litajitenga na Iraq, wale waliohusika na suala hilo watabeba dhima ya usaliti na khiana hiyo.
Ameongeza kuwa, "Wakuu wa eneo la Kurdistan badala ya kushirikiana na Marekani na utawala wa Kizayuni katika utekelezaji wa njama za 'Mashariki ya Kati Mpya' wanapaswa kukabiliana na njama hiyo."
Kura ya maoni ya kujitenga eneo la Kurdistan na Iraq ilifanyika Spetemba 25 kutokana na ubinafsi wa rais wa eneo hilo Masoud Barzani. Jamii ya kimataifa imepinga vikali kura hiyo ya maoni.
Ayatullah Imami Kashani pia ameashiria mazungumzo ya nyuklia na kusema, Iran imesimama kidete katika kadhia ya mapatano ya nyuklia na kukabiliana na siasa za kujitakia makuu za Marekani kwa sababu ya mashahidi waliojitolea wakati wa vita vya kujihami kutakatifu ambao kigezo chao kilikuwa ni mwamko wa Ashura wa Imam Hussein AS huko Karbala.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesema, Rais Donal Trump wa Marekani, wakuu wa utawala wa Kizayuni na utawala wa Aal Saud wote wamekasirishwa na ushujaa wa Iran ambao unatokana na utamaduni wa Ashura.
Huku akitoa salamu za rambi rambi katika siku hizi za kukumbuka kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS, Ayatullah Kashani amesema, Ashuraa ni funzo lenye thamani na ni itikadi ambayo inawafunza vijana wa Kiislamu kujitolea muhanga katika kukabiliana na adui.