Zarif asema Iran na Oman zina uhusiano mzuri na wa karibu
-
Sultan Qaboos bin Said Al Said wa Oman na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Jawad Zarif
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uhusiano wa Iran na Oman katika sekta za siasa, uchumi, usalama na masuala ya eneo ni mzuri na ni wa karibu.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo leo Jumatatu alasiri kabla ya kufanya mazungumzo na mfalme wa Oman, Sultan Qaboos mjini Muscat. Zarif ameongeza kuwa, uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman ni wa kipekee. Aidha amesema akiwa nchini Oman anafanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo kuhusu matukio na migogoro ya eneo la Mashariki ya Kati na pia kuhusu masuala ya uchumi na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi ya Iran hadi Oman.
Zarif pia ameashiria ushirikiano mzuri wa benki za Iran na Oman na kusema nchi hizi mbili jirani pia zinashirikiana vizuri katika sekta za utalii wa kiafya, utalii wa kidini na utalii wa kawaida.
Kuhusuiana na kadhia ya kura ya maoni ya eneo la Kurdistan kujitenga na Iraq, Zarif amesema Ufalme wa Oman una msimamo sawa na wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu udharura wa kulinda mamlaka kamili ya kujitawala Iraq na kuzingatiwa katiba ya Iraq inayosisitiza umoja wa kitaifa wa nchi hiyo. Zarif pia amesistiza udharura wa pande zote kutekeleza makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA. Amesema Oman inaunga mkono msimamo wa Iran kuhusu mapatano hayo ya nyuklia.
Baada ya kuwasili Muscat mapema leo Jumatatu, Zarif alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Yusuf Bin Alawi ambapo walijadili uhusiano wa pande mbili pamoja na masuala ya kieneo na kimataifa.