Zarif: Iran itatoa jibu mwafaka kwa misimamo ya Trump kuhusu JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i35405-zarif_iran_itatoa_jibu_mwafaka_kwa_misimamo_ya_trump_kuhusu_jcpoa
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran itatoa jibu mwafaka kujibu mapigo ya hatua yoyote ya kiuhasa itakayochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya makubaliano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 08, 2017 23:02 UTC
  • Zarif: Iran itatoa jibu mwafaka kwa misimamo ya Trump kuhusu JCPOA

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran itatoa jibu mwafaka kujibu mapigo ya hatua yoyote ya kiuhasa itakayochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya makubaliano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA.

Mohammad Javad Zarif aliyasema hayo jana Jumapili hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Iran itaendelea kutekeleza sera zake katika eneo la Mashariki ya Kati licha ya domokaya na kupayuka kwa wengine.

Dakta Zarif amebainisha kuwa: "Baada ya Trump kutekeleza msimamo wake ambao uko wazi kabisa kuhusu JCPOA, Iran itatoa jibu mwafaka na kwa wakati mwafaka."

Siku ya Jumamosi iliyopita Zarif aliiambia kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar kuwa, Marekani ina mazoea ya kuzikea vikwazo nchini nyingine, lakini baada ya kupita miongo minne chini ya vikwazo, Jamhuri ya Kiislamu imesimama kidete na kuwa na 'kinga' dhidi ya vikwazo hivyo.

Rais Donald Trump wa Marekani 

Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yametolewa baada ya gazeti la Washington Post kuripoti siku ya Alkhamisi kuwa, Trump anatazamiwa kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran eti kwa kuwa haijaonyesha 'moyo na irada' ya kuyatekeleza barabara mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Trump ambaye wakati wa kampeni zake aliyataja makubaliano ya JCPOA kuwa makubaliano mabaya zaidi kutiwa saini katika historia ya Marekani, aliapa kuyachana katika siku zake za kwanza ofisini.