Ujumbe wa Iran kwa Ulimwengu wa Kiislamu wa 'Wito wa Mazungumzo'.
Eneo la Asia Magharibi halina uwezo wa kuhimili tena mgogoro mwengine mpya. Madola ya eneo yanafahamu fika kuwa madola yaliyo nje ya eneo yanajaribu kuibua migogoro katika eneo hilo la kistratijia.
Hivi sasa kuna hatua zinazochukuliwa kujaribu kupunguza migogoro katika eneo la Asia Magharibi. Hata Saudi Arabia ambayo imekwama katika kinamasi cha Yemen nayo pia imekaribisha pendekezo la mazungumzo lililotolewa na rais wa zamani wa nchi hiyo ili kwa njia hiyo ijikwamue kistaarabu na kidiplomasia kwenye mgogoro wa Yemen.
Aidha baada ya Saudia kuibua mgogoro nchini Lebanon, hivi sasa watawala wa Riyadh wamelegeza msimamo; na kufuatia hatua ya Saad Hariri kubatilisha uamuzi wake wa kijiuzulu, moto wa mgogoro katika nchi hiyo umezimwa.
Aidha mfano mwingine ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ambaye hivi karibuni aliashiria hitilafu zilizoko katika eneo na kusema hitilafu hizo zinapasa kutatuliwa kwa njia za kidiplomasia na mazungumzo.
Hata kabla ya kuibuka vita vya ndani katika nchi kadhaa za eneo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikiunga mkono utatuzi wa migogoro ya eneo kwa njia ya mazungumzo na amani. Pamoja na kuwa Saudia imekuwa ikionyesha uhasama wa wazi na kutaka kuanzisha mzozo na Iran, lakini wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakisisitiza kuhusu ulazima wa nchi za Kiislamu kutatua matatizo yao kwa njia za mazugumzo.

Kwa mantiki hiyo,siku ya Jumamosi, Rais Hassan Rouhani wa Iran aliashiria kuwadia Wiki ya Umoja wa Kiislamu na akasisitiza kuhusu udharura wa kuhitimishwa kwa njia ya mazungumzo misuguano na mivutano katika eneo. Huu ni ujumbe ambao iwapo madola mengine katika eneo yatausikia na kuufuata basi migoroo iliyopo itamalizika na makundi yenye misimamo mikali yataangamizwa na hivyo kuandaa mazingira ya nchi za Kiislamu kubadilika na kuwa kambi yenye nguvu na ushawishi duniani.
Pamoja na hayo, ni wazi kuwa madola ya nchi za Magharibi ambayo yanaunga mkono kuwepo kwa mfumo wa kambi moja ya kimataifa pasina kuwepo kambi ya pili au ya tatu yenye uwezo na nguvu hayataruhusu kuibuka madola mengine yenye nguvu hasa ikiwa yatakuwa ni madola ya Kiislamu. Ni kwa msingi huu ndio sauti ya kuibua mifarakano inasikika kutoka kwa vibaraka wa madola ya magharibi katika eneo.
Mfano wa wazi ni Adel al Jubeir, Waziri wa Mambo ya Nje mwanagenzi wa Saudi Arabia ambaye ana dhana potovu kuwa kwa kuibua uzushi na hutuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran uthabiti utapatikana katika eneo.
Al Jubeir, ambaye aliwahi kuwa balozi wa Saudi mjini Washington, aliweza kuitumia fursa hiyo kuanzisha uhusiano wa karibu na mashirika ya kijasusi ya Marekani na hivi sasa amechukua nafasi ya mchochezi mkuu wa vita katika eneo ili kuhakikisha kuwa madola ya Kiislamu hayachukui nafasi kama kambi yenye nguvu na taathira katika dunia.
Katika hali kama hii ni wazi kuwa waliowengi katika ulimwengu wa Kiislamu wamechoshwa na vita na malumbano na wameusikia wito wa Iran wa kutaka kuwepo na mazungumzo na maelewano.
Kwa msingi huo ni kwa maslahi ya madola na wadau wote katika eneo kuweka kando chuki na uhasama na kufuata mkondo wa Umma wa Kiislamu wa umoja ili kukabiliana na njama za maadui pamoja na fikra za magaidi wakufurishaji.