SEPAH: Hatua ya Trump ni fitina kubwa dhidi ya Umma wa Kiislamu
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) limelaani hatua ya Rais wa Marekani ya kuutambua rasmi mji wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa kijahili wa Israel na kuitaja hatua hiyo kuwa fitina kubwa kwa Umma wa Kiislamu.
Rais Donald Trump wa Marekani juzi usiku aliutangaza mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa kijahili wa Israel licha ya kupingwa pakubwa kieneo na kimataifa.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) limetoa taarifa na kueleza kuwa: Hatua ya upande mmoja na kipumbavu ya Rais wa Marekani ya kuutambua mji wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa kijahili na unaouwa watoto wa Kizayuni ni fitina kubwa dhidi ya Umma wa Kiislamu na kupuuza haki za wananchi wa Palestina; na kwamba kuna ulazima Ulimwengu wa Kiislamu na taasisi nyingine zilizo huru na zinazopigania ukombozi kuchukua hatua madhubuti na za wazi ili kusambaratisha njama hiyo mbovu.
Taarifa ya jeshi la Sepah imeongeza kuwa hakuna shaka kuwa njama hizo hatari hazifasiri ndoto ya wakuu wa White House na Uzayuni wa kimataifa, bali zitaimarisha zaidi safu ya muqawama kuliko ilivyokuwa huko nyuma ili kufuatilia kukombolewa Quds Tukufu.
Sepah imesisitiza kuwa, Intifadha ya Palestina iko katika marhala mpya, na itaendeleza mwendo kasi kuliko ilivyokuwa huko nyuma kwa kuungwa mkono kwa pande zote na Umma wa Kiislamu.