Hossein Amir-Abdollahian: Iran inakitetea kibla cha kwanza cha Waislamu
Hossein Amir-Abdollahian, msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, Iran daima imekuwa mtetezi wa haki za wananchi madhulumu wa Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu na itaendelea kufanya hivyo.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake na Saud bin Ahmad al-Barwani balozi wa Oman hapa mjini Tehran ambapo ameashiria hatua ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitangaza Beitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel na kusema kwamba, Quds ni mali ya Ulimwengu wa Kiislamu na nchi zote za Kiislamu na kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa pamoja na nchi nyingine za kiislamu inapinga vikali kutekelezwa kivitendo kwa uamuzi huo wa Trump.
Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema hayo katika hali ambayo upinzani na malalamiko dhidi ya hatua ya Rais Trump wa Marekani ya kuitangaza Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa Israel yanaendelea kushuhudiwa kila kona ya dunia.
Aidha Hossein Amir-Abdollahian,ameashiria uhusiano mkongwe wa Iran na Oman na kueleza kwamba, kuna uhusiano mzuri na wa kirafiki baina ya nchi mbili hizi katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wake Saud bin Ahmad al-Barwani balozi wa Oman hapa mjini Tehran amekaribisha kwa mikono miwili kuongezwa ushirikiano kati ya Tehran na Muscut.
Kadhalika balozi wa Oman mjini Tehran amesisitiza juu ya kupatiwa ufumbuzi matatizo ya Mashariki ya Kati kupitia njia ya mazungumzo na ufumbuzi wa kisiasa.