Larijani: Vita athirifu dhidi ya ugaidi vinategemea umoja wa nchi za eneo
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, vita athirifu dhidi ya ugaidi vinategemea umoja na mshikamano wa nchi za eneo katika suala hilo.
Dakta Ali Larijani amesema hayo leo mjini Islamabad Pakistan baada ya mazungumzo yake kwa nyakati tofauti na Maspika wa Mabunge wa nchi zinazoshiriki katika mkutano wa "Changamoto za Kukabiliana na Ugaidi na Nafasi ya Ushirikiano wa Kieneo" ambapo ameashiria nafasi muhimu na athirifu ya umoja wa nchi za eneo katika kupambana na kundi la kigaidi la Daesh nchini Syria na Iraq na kusema kwamba, umoja huo umesambaratisha njama kubwa za kuimarisha ugaidi katika Mashariki ya Kati.
Dakta Larijani amesema kuwa, mkutano ujao wa kujadili namna ya kupambana na uugaidi utafanyika mjini Tehran mwaka ujao na kusema kuwa, katika kipindi hiki cha kabla ya mkutano huo kutafanyika juhudi za kutafuta mbinu bora za kupambana na makundi ya kigiadi na kuandaa uwanja wa kupatikana amani na uthabiti katika eneo la Masharikki ya Kati.
Ajenda nyingine zilizojadiliwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo yake na Maspika wa Mabunge wa nchi nyingine zinazoshiriki mkutano huo ni suala la uwekekezaji vitega uchumi nchini Iran.
Mkutano wa "Changamoto za Kukabiliana na Ugaidi na Nafasi ya Ushirikiano wa Kieneo" ulianza jana Jumapili mjini Islamabad kwa ubunifu wa Bunge la Taifa la Pakistan na kuhudhuriwa na Maspika wa Bunge kutoka nchi sita za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, Afghanistan, Uturuki, China na mwenyeji Pakistan.