Magari yaliyotengenezwa nchini Iran kuanza kuuzwa nchini Oman
Mkuu wa kitengo cha biashara katika ubalozi wa Iran mjini Muscat amesema magari yaliyotegenezwa katika viwanda vya Iran sasa yataanza kuuzwa katika soko la Oman.
Abbas Abdul-Khani mwambata wa biashara katika ubalozi wa Iran nchini Oman amesema: "Shirika la kutengeneza magari la Iran Khodro kama shirika la kwanza la utengenezaji magari Iran, limepata kibali cha viwango cha (GSO) cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na hivyo kuidhinishwa kuuza magari yake Dena Plus na Runna katika eneo."
Abdul-Khani ameongeza kuwa, baada ya majaribio yaliyofana, magari hayo mawili ya Iran sasa yamepata idhini ya kuuzwa katika soko la nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ambazo mbali na Oman ni Kuwait, Qatar, Bahrain, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Ametabiri kuwa magari ya Iran yataweza kuwavutia watu wengi katika nchi hizo za Kiarabu kutokana na viwango vya juu vilivyotumiwa katika kuyatengeneza.
Oman ni nchi ya 10 inayonunua bidhaa za Iran kwa wingi duniani na katika miezi ya kwanza minane ya mwaka huu nchi hiyo jirani ya Kiarabu imenunua bidhaa zenye thamani ya dola milioni 368 kutoka Iran.
Iran ina uhusiano mzuri na wa kidugu na Oman katika sekta za siasa, uchumi na utamaduni.