Stratijia mpya ya ulinzi wa Marekani, kukaririwa madai bandia dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39289-stratijia_mpya_ya_ulinzi_wa_marekani_kukaririwa_madai_bandia_dhidi_ya_iran
Ijumaa iliyopita Jim Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani aliwasilisha waraka mpya wa stratijia za ulinzi za taifa la Marekani katika mwaka huu wa 2018.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 21, 2018 23:33 UTC
  • Stratijia mpya ya ulinzi wa Marekani, kukaririwa madai bandia dhidi ya Iran

Ijumaa iliyopita Jim Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani aliwasilisha waraka mpya wa stratijia za ulinzi za taifa la Marekani katika mwaka huu wa 2018.

Katika waraka huo sawa na waraka wa stratijia ya usalama wa taifa la Marekani uliotolewa mwezi Disemba mwaka jana, katika ngazi ya kimataifa, nchi mbili za Russia na China zilitajwa kuwa tishio kwa Marekani, huku waitifaki wao katika ngazi ya kieneo yaani Iran na Korea Kaskazini pia, zikitajwa kuwa changamoto kuu kwa Washington. Katika muhtasari wa waraka huo wenye kurasa 11 wa stratijia za ulinzi wa taifa la Marekani, jina la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetajwa mara sita. Ukweli ni kwamba waraka huo badala ya kuitwa stratiji ya ulinzi wa taifa, ulitakiwa kuitwa kwa jina la stratijia ya hujuma ya kitaifa ya Marekani, hasa kutokana na tuhuma zisizo na msingi zilizokaririwa na Washington dhidi ya Iran ya Kiislamu.

Sehemu ndogo ya makombora ya Iran yanayoitia kiwewe Marekani, Saudia na Israel

Miongoni mwa tuhuma hizo dhidi ya Tehran ni zile za zamani kwamba eti Iran ni chimbuko la ukatili, changamoto muhimu kwa ajili ya usalama wa eneo la Mashariki ya Kati, kuwa na mpango wa kuunda silaha za nyuklia na kuunga mkono ugaidi na kwamba mambo hayo ndiyo yamelifanya eneo hili kukosa usalama kutokana na ushawishi wa lran ndani ya eneo hili. Aidha katika waraka huo, imeelezwa kwamba Pentagon itaendeleza juhudi zake kwa ajili ya kuisambaratisha Iran. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Pentagon inakusudia kutekeleza mpango huo kupitia kuundwa muungano wa kieneo dhidi ya Tehran. Tuhuma zilizotajwa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) dhidi ya Iran ya Kiislamu, ni zile zile ambazo zimekuwa zikifuatiliwa kwa miaka mingi na Washington katika eneo la Mashariki ya Kati ambapo kupitia mpango huo Marekani inajaribu kuuonyesha ulimwengu, kinyume na ukweli wa mambo ulivyo, kuwa Washington ndio muungaji mkono mkubwa wa usalama na amani katika eneo hili.

Trump na Netanyahu

Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa Rais Donald Trump mwenyewe, serikali iliyopita ya Marekani chini ya Rais Barack Obama, ndiyo iliyounda kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) kwa ajili ya kudhamini malengo ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, huku washirika wa Washington wa Kiarabu hususan utawala wa Aal-Saud nchini Saudia ukiwa muungaji mkono mkubwa wa kundi hilo la Kiwahabi. Ikiwa kusudio la Marekani la eti kuenezwa ushawishi na kuvurugwa usalama wa Mashariki ya Kati unaofanywa na Iran, ni muqawama ambao kiuhalisia unahesabiwa kuwa ni tishio kubwa kwa uwepo wa utawala bandia wa Kizayuni, basi hilo ni jambo ambalo daima Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikilisisitizia na kuliunga mkono. Amma kuhusiana na  miradi ya makombora yake pia, Iran imekuwa ikitangaza mara kwa mara kwamba, miradi yake ya makombora ni kwa ajili ya kujilinda kutokana na vitisho vya maadui wake na kimsingi Tehran haina lengo la kutekeleza hujuma za kijeshi na kichokozi dhidi ya nchi yoyote ile. Kuhusiana na suala hilo, Dave Zakem, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Marekani amekiri kwamba, kinyume na Marekani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio imekuwa muhanga wa hujuma na vita vya maadui. 

Trump na Mfalme Salman wa Saudia

Hii ni katika hali ambayo kwa upande wake Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitekeleza hatua na mipango ya kusambaratisha njama za  uhasama wa Marekani na washirika wake katika eneo. Katika uwanja huo Harry Kazianis, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa Marekani anaamini kwamba, huu sio wakati wa kukabiliana na Iran kijeshi na kwa hakika suala hilo halitakiwi kufikiriwa hata kidogo na timu ya Trump, kwani kujaribu kosa hilo hakutakuwa na faida kwa Washington ghairi ya kuidhoofisha Marekani katika kukabiliana na matatizo makubwa zaidi. Alaa kulli hal, hivi sasa Iran inakabiliana na siasa haribifu za Washington na washirika wake katika eneo hususan utawala wa Aal-Saud na utawala wa Kizayuni wa Israel, suala ambalo limeikasirisha sana Marekani  na kuifanya iendelee kubuni njama na mipango hasimu na ya kichochezi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya lran.