Qassemi: Iran haitafanya mazungumzo na yeyote kuhusu miradi yake ya makombora
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i39329-qassemi_iran_haitafanya_mazungumzo_na_yeyote_kuhusu_miradi_yake_ya_makombora
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haijafanya na haitafanya mazungumzo na nchi yoyote ile kuhusiana na mpango wake wa makombora.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 22, 2018 11:00 UTC

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haijafanya na haitafanya mazungumzo na nchi yoyote ile kuhusiana na mpango wake wa makombora.

Bahram Qassemi amesema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari leo na kusisitiza kuwa, Iran imesema na kusisitiza mara chungu nzima kwamba, mpango wake wa makombora si jambo la kufanyiwa mazungumzo.

Bahram Qassemi amesema pia kwamba, katika safari ijayo ya Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa hapa mjini Tehran, pande mbili zitajadili masuala kadhaa ya kisiasa yakiwemo ya kieneo na kimataifa na kubadilishana mawazo katika uwanja huo.

Moja ya makombora ya Iran likifanyiwa majaribio

Akijibu swali kuhusiana na madai ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa kwamba, akiwa hapa nchini atafanya mazungumzo na viongozi wa Tehran kuhusiana na ushawishi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati, uungaji mkono wake kwa Hizbullah ya Lebanon na Yemen amesema kuwa, safari ya Jean-Yves Le Drian hapa nchini imepangwa tayari lakini ajenda hasa za mazungumzo hayo bado hazijafahamika.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu amezungumzia taarifa za baadhi ya vyombo vya habari kuhusiana na kuuweko mazungumzo baina ya Marekani na Ulaya kwa ajili ya kuiwekea vikwazo zaidi Tehran na kusema kuwa, huo ni mjadala wa vyombo vya habari, lakini ukweli hasa wa mambo ni kwamba, uhusiano wa Iran na nchi za Uulaya upo katika hali nzuri na katika mkondo wa kukua.