Zarif: Trump anawasilisha ushahidi bandia dhidi ya Iran katika Baraza la Usalama
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Rais Donald Trump wa Marekani anategemea ushahidi bandia kueneza chuki dhidi ya Iran duniani.
Kupitia ujumbe kwa njia ya Twitter siku ya Jumatatu, Zarif amesema: "Katika kitengo cha habari bandia, Trump na wenzake wanajaribu kueneza riwaya ya chuki dhidi ya Iran (Iranophobia) katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Wanaitisha dhifa na kuwasilisha ushahidi bandia walioupata kutoka kwa jirani anayeeneza vita."
Zarif amesema propaganda kama hizo zitakubaliwa tu na 'huyo jirani anayetapatapa na ambaye ametanda jinai za kivita". Zarif hapo alikuwa akiashiria Saudi Arabia ambayo iko mstari wa mbele katika kutekeleza njama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kauli ya Zarif imekuja baada ya Rais wa Marekani kuhutubia dhifa ya mabalozi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walioalikwa katika Ikulu ya White House ambapo alikariri tuhuma kuwa eti Iran inavuruga uthabiti wa Mashariki ya Kati na kwamba eti inawapa makombora ya balistiki wapiganaji wa Ansarullah nchini Yemen.
Mnamo Disemba 14 Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley aliwasilisha kile alichodai kuwa eti ni ushahidi kuwa Iran imewapa wapiganaji wa Ansarullah makombora ambayo yametumika kuilenga Saudi Arabia. Wapiganaji wa Ansarullah na wanajeshi wa Yemen, tokea mwaka 2015 wamekuwa wakikabiliana na hujuma ya kinyama ya Saudia na waitifaki wake dhidi ya nchi hiyo.