Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu: Kuwepo Iran katika eneo hili hakuipendezi hata kidogo Marekani
(last modified Fri, 09 Mar 2018 06:25:44 GMT )
Mar 09, 2018 06:25 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu: Kuwepo Iran katika eneo hili hakuipendezi hata kidogo Marekani

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha wazi kwamba taifa la Iran liko tayari muda wote kumpigisha magoti adui yake na kusisitiza kuwa, uwepo wa Iran katika eneo hili hauihusu kivyovyote vile Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema hayo jana Alkhamisi wakati alipoonana na maelfu ya malenga na wasomaji kasida za Ahlul Bayt watoharifu AS na huku akiashiria namna viongozi wa Marekani na wa Ulaya wanavyoiomba Iran ifanye mazungumzo nao kuhusu uwepo na ushawishi wake katika eneo hili na kusema kuwa: Wakati ambapo Marekani inafanya uharibifu na kueneza fitna katika kila kona ya dunia, (yote hayo inayaacha na badala yake) muda wote inafanya chokochoko kuhusu uwepo wa Iran katika eneo hili. Ayatullah Khamenei aidha amebainisha kwamba Iran haihitajii kuzungumza na madola ajinabi ya kibeberu kuhusu uwepo wake katika eneo hili, bali yenyewe inazungumza moja kwa moja na nchi za eneo hili na kuwaambia viongozi wa Marekani kuwa: Wakati wowote tutakapohisi kuna haja ya sisi kuweko huko Marekani tutakuja kuzungumza na nyiyi! Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia ombi la viongozi wa Ulaya ambao wanasema wanapenda kufanya mazungumzo na Iran kuhusu uwepo wake katika eneo hili na kubainisha kuwa, watu wa Ulaya haliwahusu kivyovyote vile suala la kuwepo Iran katika eneo hili.

Mapenzi ya wananchi wa Syria kwa Iran

 

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na nafasi muhimu huru katika eneo hili na kwenye maamuzi na mambo yake yote na haishughulishwi na Wamarekani wala Wazungu wa Ulaya katika maamuzi yake ya kulinda manufaa yake na ya mataifa ya eneo hili la kiistratijia la Asia Magharibi. Siasa kuu za Iran zimejengeka juu ya msingi wa kuishi kwa usalama na amani na majirani zake na kutatua matatizo yanayojitokeza kwa njia ya mazungumzo ya kiuadilifu baina ya pande zote husika. Vile vile Iran inafuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa na kiusalama ya eneo lake hili na kutoa msaada haraka popote inapoombwa kufanya hivyo. Siasa kuu za Iran ni kutatua masuala ya eneo hili kwa njia ya mazungumzo na kwa ajili ya kuleta usalama wa kudumu bila ya uingiliaji wa madola baki yanayotoka nje ya eneo hili. Pendekezo la Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran la kuundwa baraza la kieneo la mazungumzo, lengo lake ni kutatua matatizo yaliyopo kwenye eneo hili kwa njia ya mazungumzo na kwamba pendekezo hilo linaonesha namna Iran ilivyo na nia njema na inavyolipa umuhimu suala la kushirikiana nchi za eneo hili kutatua matatizo yao kwa njia za amani na kutoruhusu uchochezi wa madola ajinabi ambayo hayana nia njema hata chembe na watu wa janibu hii.

Kusambatishwa khilafa bandia ya Daesh huko Iraq na Syria ni matunda ya uwepo imara na wa mahala pake kabisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la Asia Magharibi. Ushirikiano mzuri na wa kisheria wa Iran na nchi za Iraq na Syria umebatilisha njama za Magharibi hususan Marekani katika eneo hili. Kuyajali mataifa ya eneo hili na kuyasaidia kukabiliana na maadui zao ni jukumu la dhati la Iran ambayo ni nchi yenye taathira katika matukio ya eneo hili. Mafanikio iliyopata hivi sasa kambi ya muqawama, kuanzia Lebanon hadi Syria, Iraq na Yemen ni kigezo kizuri cha ushirikiano wa kieneo ambao unazidi kupanuka. Ushirikiano huo imara na wenye malengo maalumu umepiga kengele ya hatari kwa manufaa haramu ya nchi za Ulaya na Marekani na ndio maana sasa nchi hizo zimezuka na ombi la kutaka kuzungumza na Iran kuhusu uwepo na ushawishi wake katika eneo hili.

Mapenzi ya wananchi wa Palestina kwa Iran. Bango hilo katika moja ya barabara kuu za Ghaza, Palestina

 

Nchi za Magharibi hususan Ufaransa, Uingereza na Marekani zinaeneza propaganda chafu kwamba eti uwepo wa Iran unasababisha uharibifu kwenye eneo hili katika hali ambayo magenge tofauti ya kigaidi yaliyofanya jinai na yanayoendelea kufanya jinai katika nchi za eneo hili hususan huko Syria yameanzishwa na kupewa mafunzo ya kijeshi pamoja na silaha na madola hayo hayo ya Magharibi. Ukweli wa mambo ni kuwa madola hayo ya Magharibi yanakasirishwa na jinsi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inavyosambaratisha njama zao katika eneo hili na haziwezi kufanya chochote kwani ni kama alivyosisitiza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba: Taifa la Iran liko imara na liko tayari wakati wowote kumrejesha huko huko alikotoka mvamizi na adui yeyote yule. 

Tags