Zarif: Ushiriki mkubwa wa Marekani katika maafa ya Yemen hautasawariki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i42390-zarif_ushiriki_mkubwa_wa_marekani_katika_maafa_ya_yemen_hautasawariki
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amekosoa nafasi kubwa ya Marekani katika vita na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen na kusisitiza kuwa, ushiriki mkubwa wa Washington katika maafa makubwa zaidi ya binadamu duniani hautasawariki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 29, 2018 23:34 UTC
  • Zarif: Ushiriki mkubwa wa Marekani katika maafa ya Yemen hautasawariki

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amekosoa nafasi kubwa ya Marekani katika vita na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen na kusisitiza kuwa, ushiriki mkubwa wa Washington katika maafa makubwa zaidi ya binadamu duniani hautasawariki.

Katika ujumbe wake uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Muhammad Javad Zarif ameashiria misaada ya silaha ya Marekani kwa Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen na kusema kwamba: "Inaonekana Marekani haitosheki na kuipatia Saudia mabomu, kulenga shabaha na kuzipa mafuta ndege za kijeshi za Saudia." 

Dakta Zarif amesema sasa Marekani inasema inashiriki kupanga na kusimamia mashambulizi dhidi ya watu wa Yemen na kuongeza kuwa: "Kiwango kikubwa cha ushiriki wa Marekani katika maafa makubwa zaidi ya binadamu duniani hakiwezi kutasawarika."

Watoto wa Yemen, wahanga wakuu wa mashambulizi ya Saudia

Machi mwaka 2015 Saudi Arabia na washirika wake wakisaidiwa na Marekani, Israel na nchi nyingine kadhaa zilianzisha mashambulizi ya kila upande dhidi ya Yemen kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani rais aliyejiuzulu na kutoroka nchi wa nchi hiyo, Abdrabbuh Mansur Hadi. Maelfu ya raia wa Yemen wameuawa katika vita hivyo ambavyo sasa vimeingia katika mwaka wake wa nne na ripoti za Umoja wa Mataifa zinasema zaidi ya asilimia 80 ya miundombinu ya nchi hiyo imeharibiwa kwa mashambulizi ya Saudia.