Iran yaionya Ufaransa isikubali kulaghaiwa na Bin Salman kuhusiana na Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i43026-iran_yaionya_ufaransa_isikubali_kulaghaiwa_na_bin_salman_kuhusiana_na_syria
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, viongozi wa serikali ya Ufaransa wanapaswa kuwa macho na wasikubali kurubuniwa na madai ya uongo na propaganda za Mohammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia ambaye ni mwanagenzi sana katika masuala ya siasa na vita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 13, 2018 00:06 UTC
  • Iran yaionya Ufaransa isikubali kulaghaiwa na Bin Salman kuhusiana na Syria

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, viongozi wa serikali ya Ufaransa wanapaswa kuwa macho na wasikubali kurubuniwa na madai ya uongo na propaganda za Mohammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia ambaye ni mwanagenzi sana katika masuala ya siasa na vita.

Qassemi alisema hayo jana jioni katika kujibu ripoti ya pamoja ya Saudia na Ufaransa iliyotolewa mwishoni mwa safari ya mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia nchini Ufaransa ambapo katika taarifa hiyo, nchi hizo ziliituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema kuwa Ufaransa kama nchi mwanachama wa kundi la 5+1 haitakiwi kuatahiriwa na maneno, tuhuma za mara kwa mara na za uongo na ghilba za Saudia zinazoichochea Ufaransa isiheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akiwa na Mohammd Bin Salman mjini Paris

Aidha Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, kinyume na madai yaliyotolewa na Ufaransa na Saudia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kuleta utulivu na usalama katika nchi za Mashariki ya Kati sambamba na kupambana na ugaidi. Bahram Qassemi amesisitiza kuwa Tehran inaamini kwamba mazungumzo ndiyo njia pekee ya kurejesha usalama na amani katika eneo la magharibi mwa Asia. Akibainisha kwamba makombora ya Iran ni kadhia ya ndani ya nchi amesema kuwa, viongozi wa Ufaransa wanatakiwa kufahamu kwamba, mpango wa makombora wa ya Iran ni suala lisilopasa kujadiliwa kabisa kwani linahusiana na kujilinda Iran kama ilivyo kwa nchi zote nyingine. 

Baadhi ya makombora ya Iran yanayoitia kiwewe Magharibi

Kadhalika Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa madai ya pamoja ya Ufaransa na Saudia ya kwamba eti Tehran inatuma silaha zake nje ya nchi kwenda kwa makundi ya eneo la Mashariki ya Kati na kusema kuwa, viongozi wa Ufaransa wanatakiwa kuacha kupotosha fikra za walio wengi na kuachana na siasa za kuipatia silaha zake Saudia, silaha ambazo hadi sasa zimetumika kuua raia wengi wasio na hatia huko Yemen.