Zarif aonya kuhusu tishio la misimamo ya kufurutu ada Mashariki ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i43278-zarif_aonya_kuhusu_tishio_la_misimamo_ya_kufurutu_ada_mashariki_ya_kati
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametahadharisha kuhusu tishio la misimamo mikali ya kufurutu ada katika eneo licha ya kuangamizwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Apr 17, 2018 23:49 UTC
  • Zarif aonya kuhusu tishio la misimamo ya kufurutu ada Mashariki ya Kati

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametahadharisha kuhusu tishio la misimamo mikali ya kufurutu ada katika eneo licha ya kuangamizwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Mohammad Javad Zarif aliyasema hayo jana Jumanne akihutubia mkutano wa 23 wa mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ECO, mjini Dushanbe nchini Tajikistan.

Dakta Zarif amebainisha kuwa, "misimamo ya kuchupa mipaka ingali tishio katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi. Licha ya kuzimwa genge la kigaidi la Daesh na makundi mengine ya kigaidi katika eneo, lakini mitandao ya makundi yenye misimamo ya kufurutu ada katika maeneo ya magharibi, kusini na katikati mwa Asia ingali tishio kubwa kwa usalama eneo la ECO."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitizia udharura wa kuundwa stratejia ya pamoja ya kieneo, kwa shabaha ya kuzuia kuenea aidiolojia ya ugaidi na utakfiri, sambamba na kukata vyanzo vyote vya fedha vya makundi hayo.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa ECO

Ameongeza kuwa, ukuruba wa kijiografia na kufanana kwa mambo mengi miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi kama vile utamaduni, ustaarabu, dini na historia, ni mambo yanayoweza kutumiwa kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama wa ECO.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ECO iliundwa mwaka 1985 na Iran, Pakistan na Uturuki, na kisha mwaka 1992 ikapanua wigo wake na kuzijumuisha nchi nyingine saba za Afghanistan, Azerbaijan, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan.