Zarif: Uingiliaji wa maajinabi umechelewesha kupatikana suluhu na amani nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i43648-zarif_uingiliaji_wa_maajinabi_umechelewesha_kupatikana_suluhu_na_amani_nchini_syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema, uingiliaji wa maajinabi umechelewesha kupatikana suluhu na amani nchini Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 25, 2018 22:51 UTC
  • Zarif: Uingiliaji wa maajinabi umechelewesha kupatikana suluhu na amani nchini Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema, uingiliaji wa maajinabi umechelewesha kupatikana suluhu na amani nchini Syria.

Dakta Zarif ameyasema hayo katika mkutano wa pili wa Umoja wa Ulaya kuhusu Syria uliofanyika jana kwenye makao makuu ya umoja huo mjini Brussels, Ubelgiji.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, kipaumbele kikuu nchini Syria ni kusimamishwa vita na akabainisha kwamba Iran, kwa kushirikiana na Russia na Uturuki, zikiwa ni nchi zinazosimamia mchakato wa mazungumzo ya Astana zinafanya jitihada ya kupanua wigo wa maeneo yasiyo na mivutano na mapigano nchini Syria.

Zarif ameongeza kuwa mchakato huo umeanzishwa kwa msingi kwamba mgogoro wa Syria unaweza kutatuliwa kwa njia ya kisiasa tu, katika sura ya mchakato wenye uhalisia na wigo mpana wa kisiasa utakaoongozwa na kuwa chini ya mamlaka ya wananchi wenyewe wa Syria na kwa msingi wa kuheshimiwa kikamilifu mamlaka ya kujitawala, uhuru na umoja wa ardhi yote ya nchi hiyo.

Amebainisha pia kwamba katika kipindi chote cha miaka ya karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kutuma misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Syria wakiwamo wakimbizi wa ndani na watu waliowekewa mzingiro.

Mkuu wa Sera za Nje wa EU Federica Mogherini ni mmoja wa shakhsia waliohutubia mkutano wa Brussels 

Mkutano wa pili wa Umoja wa Ulaya kuhusu Syria uliofanyika jana mjini Brussels umehudhuriwa na viongozi na maafisa kutoka nchi 80 duniani ikiwamo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mkutano huo umefanyika chini ya uenyekiti wa pamoja wa umoja huo na Umoja wa Mataifa.

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa hujuma na mashambulio makubwa na ya kila upande ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao kwa lengo la kubadilisha hali ya mlingano wa eneo la Mashariki ya Kati kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni wa Israel.../