Zarif: Usalama wa Ghuba ya Uajemi unapasa kudhaminiwa na nchi za eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i43862-zarif_usalama_wa_ghuba_ya_uajemi_unapasa_kudhaminiwa_na_nchi_za_eneo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa Ghuba ya Uajemi ni eneo muhimu ambalo usalama wake unapaswa kudhaminiwa na mataifa ya eneo hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 30, 2018 09:46 UTC
  • Zarif: Usalama wa Ghuba ya Uajemi unapasa kudhaminiwa na nchi za eneo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa Ghuba ya Uajemi ni eneo muhimu ambalo usalama wake unapaswa kudhaminiwa na mataifa ya eneo hili.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika ujumbe wake kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Ghuba ya Uajemi ambayo imeadhimishwa leo Aprili 30. Zarif ameongeza kuwa, njia ya kivitendo ya kuunda Jumuiya ya Mazungumzo ya Kieneo ndio njia pekee ya kuleta hali ya kuaminiana katika eneo.

Leo, 30 Aprili 2018 inasadifiana na kumbukumbu ya kutimuliwa mkoloni Mreno kutoka maji ya kusini mwa Iran mnamo mwaka 1622 Miladia na inatambuliwa kama Siku ya Kitaifa ya Ghuba ya Uajemi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, "Ghuba ya Uajemi si maji tu bali ni turathi ya kihistoria yenye thamani ambayo imetufikia kutoka mababu zetu walioishi katika eneo hili."

Zarif ameongeza kuwa, Ghuba ya Uajmi ni kitovu cha thamani za kiutamaduni za kudumu za wenyeji na ni utambulisho na uhai wa Asia Magharibi.

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Ghuba ya Uajemi tokea jadi imekuwa ni njia muhimu ya kudhamini nishati na biashara ya dunia.