Shirika la Renault: Tutabakia nchini Iran licha ya vikwazo vya Marekani
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutengeneza magari la Renault la Ufaransa amesema kuwa shirika hilo litaendelea kufanya shughulia zake nchini Iran licha ya kurejeshwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Carlos Ghosn amesema hayo katika kikao cha kila mwaka cha wawekezaji wa shirika hilo na kuongeza kuwa, kamwe hawataondoka nchini Iran hata kama watalazimika kupunguza shughuli zao.
Mwaka 2017 shirika la kutengeneza magari la Renault la Ufaransa liliwekeana saini na Iran mkataba wenye thamani ya dola milioni 780.
Iran ni soko la tatu kwa ukubwa la magari na vifaa vinavyozalishwa na shirika la Renault baada ya Ufaransa na Brazil.
Rais wa Marekani Donald Trump tarehe 8 Mei mwaka huu alirejea kutoa tuhuma za uongo dhidi ya Iran na kuitoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na pia kurejesha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Tehran.
Baada ya hapo aliyapa mashirika ya kigeni yanayofanya shughuli zake nchini Iran muda wa miezi mitatu hadi 6 kuondoka nchini Iran. Alidai kuwa mashirika ya kigeni yanayoshirikiana na Iran hatafungiwa kuuza bidhaa zao katika soko la Marekani au litawekewa vikwazo na Washington.
Hatua hiyo ya kijuba ya Marekani inaendelea kulaaniwa kote ulimwenguni hasa kwa jeuri yake ya kuilazimisha dunia nzima ifuate siasa zake za kibeberu bila ya kujali uhuru wa kujitawala wa nchi hizo.