Iran na Oman zazidi kuimarisha ushirikiano wao wa baharini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i46384-iran_na_oman_zazidi_kuimarisha_ushirikiano_wao_wa_baharini
Kikao cha 17 cha kamati ya pamoja ya uchumi baina ya Iran na Oman kimehimiza kuimarishwa ushirikiano wa nchi mbili kupitia bandari ya Chabahar katika mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 27, 2018 03:29 UTC
  • Iran na Oman zazidi kuimarisha ushirikiano wao wa baharini

Kikao cha 17 cha kamati ya pamoja ya uchumi baina ya Iran na Oman kimehimiza kuimarishwa ushirikiano wa nchi mbili kupitia bandari ya Chabahar katika mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran.

Shirika la habari la ISNA limemnukuu Abdul Rahim Kurdi, mkurugenzi mkuu wa shirika la eneo huru  kibiashara la Chabahar akiashiria kikao hicho na kuongeza kuwa, ushirikiano wa kibiashara wa Iran na Oman unazidi kuimarika kupitia bandari hiyo ya kusini mashariki mwa Iran.

Amesema, uwekezaji wa pamoja, kudhaminiwa mahitajia ya chakula na mifugo, ushirikiano katika uvuvi wa baharini na kustawisha sekta ya uchukuzi na usafiri wa baharini baina ya bandari ya Sohar wa Oman na Chabahar ya Iran ndiyo yaliyokuwa masuala makuu yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho.

Katika kipindi hiki nyeti ambacho ulimwengu wa Kiislamu unapitia ndani yake, nchi mbili ndugu za Iran na Oman zimekuwa mara kwa mara zikiimarisha zaidi ushirikiano wao. Nchi hizo zina misimamo ya pamoja katika masuala mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu kiasi kwamba nchi kama Saudi Arabia na Imarati zinaiona Oman kuwa ni kizuizi kikubwa cha kufikia malengo yao.