Velayati: Iran haiondoki Syria kwa vitisho vya Marekani
Mshauri wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa amesisitiza kuwa Iran na Russia zitaendelea kuwepo huko Syria na kwamba Iran haitaondoka nchini humo kwa vitisho vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Akizungumza Ijumaa hii katika Akademia ya Valdai mjini Moscow Russia, Ali Akbar Velayati ameongeza kuwa iwapo Iran na Russia zitaondoka huko Syria; kwa mara nyingine tena magaidi wataikalia kwa mabavu nchi hiyo na kwamba kuwepo nchi mbili hizo kunatoa hakikisho la kutokuwepo tena harakati za magaidi nchini Syria.
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa amesema kuwa: Washauri wa kijeshi wa Iran wapo Syria na Iraq kufuatia ombi la serikali za nchi hizo na kwa mujibu wa sheria.
Dakta Velayati amesema Iran haitaki kufanya mazungumzo na Marekani kwa sababu nchi hiyo haiaminiki. Amesema, Iran inazuia kugawanywa nchi ya Syria kama ilivyofanyika huko Libya na wakati huo huo inaisadia Syria kukabiliana na chokochoko za Marekani.
Dakta Velayati amesema Marekani imeitaka Iran iondoke huko Syria lengo likiwa ni kutoa pigo kwa umoja ulioko baina ya Moscow na Tehran na kusisitiza kuwa Iran, Syria, Russia na harakati ya Hizbullah ya Lebanon zinachukau hatua huko Syria kwa pamoja na kwa ushirikiano.