Mtazamo wa Kiongozi; Mustakabali wa Mafanikio wa Mapinduzi ya Kiislamu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hivi karibuni alitembelewa na ujumbe wa wanaharakati wa kiutamaduni walioko nje ya nchi. Akizungumzia wasiwasi uliobainishwa na ujumbe huo kuhusu mustakabali wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei alisema:"Hawathubutu kufanya upuuzi wowote ule; waambieni hili watu wote."
Hivi karibuni, wanaharakati kadhaa wa masuala ya kiutamaduni kutoka nje ya nchi walionana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambapo mmoja wa hadhirina alibainisha dukuduku na wasiwasi walionao wapenzi wa Mapinduzi ya Kiislamu walioko nje ya mipaka ya Iran.
Alipozungumzia dukuduku na wasiwasi ulioonyeshwa na mwanaharakati huyo kutokana na hatua na njama zinazofanywa na maadui, Ayatullah Khamenei alisema:" Kuhusiana na hali yetu msiwe na wasiwasi asilani; hakuna mtu yeyote atakayethubutu kufanya upuuzi wowote ule; kuweni na uhakika kwamba hakuna shaka yoyote kuhusiana na hili; waambieni hili watu wote."
Msimamo huo imara na madhubuti wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao umetangazwa katika siku hizi ambapo serikali ya sasa ya Marekani imeanza kutekeleza awamu ya kwanza ya vikwazo dhidi ya Iran, unafikisha ujumbe wa wazi kwa viongozi wa Marekani na vibaraka wao wa eneo.
Sambamba na kuanza kutekelezwa awamu ya mwanzo ya vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Iran, rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumanne aliandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kwamba: "hivi ni vikwazo vikali zaidi kuwahi kuwekwa hadi sasa." Sera za serikali ya Trump baada ya kujitoa kwenye makubaliano ya kimataifa ya nyuklia JCPOA ni kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran, kubadilisha mwenendo wa Iran kuhusiana na masuala ya eneo na kuchochea na kushadidisha manung'uniko ndani ya nchi kwa tamaa kwamba, ndoto ambayo Marekani imekuwa ikiiota kwa miaka 40 sasa itathibiti. Uungaji mkono wa serikali ya Trump kwa genge la kigaidi la Munafikina (MKO) kwa ajili ya kufikia malengo yake na kushabikia na kuunga mkono watu wanaozusha fujo na machafuko nchini vinathibitisha upeo wa chuki na kinyongo ilichonacho Marekani kwa Mapinduzi ya Kiislamu.
Lengo hasa la Trump, kwa uungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya waarabu wanaojipendekeza kwa Marekani ukiwemo utawala wa Saudi Arabia, ni kusimamisha mpango wa makombora wa Iran, kuhitimisha uwepo, ushawishi na satua ya Iran katika eneo; na kwa kushadidisha mashinikizo, hatimaye kuhakikisha Jamhuri ya Kiislamu haiwezi kuuza nje hata tone moja la mafuta yake. Sera na siasa hizo za kihasama ni ishara ya uadui wa kihistoria dhidi ya nchi ambayo si hali yake ya huko nyuma, ya sasa wala ya mustakabali yenye utegemezi wowote ule kwa madola ya utumiaji mabavu yanayojifanya wababe wa dunia. Serikali ya Trump, kama zilivyokuwa serikali zilizotangulia za Marekani, inataka kuyakengeusha katika njia yake Mapinduzi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambao tajiriba ya miaka 40 ya uhai wake imerasimisha msingi mmoja mkuu; nao ni kuendelea kuwa "ngangari" na yenye "nguvu endelevu" mapinduzi hayo ya wananchi, yenye thamani na utambulisho maalumu.
Mnamo tarehe 21 Juni mwaka huu, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alihutubia hadhara ya mabalozi, maafisa na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje, ambapo alizungumzia, pamoja na mambo mengine, ukubwa wa uadui wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kusema: "Inachotafuta Marekani ni kurejea kwenye nafasi iliyokuwa nayo nchini Iran kabla ya Mapinduzi, na haitoridhia kingine chochote kile ghairi ya hili".
Katika mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alibainisha pia kwamba upinzani wa Washington kwa "uwezo wa kinyuklia, kuwa na utaalamu wa kurutubisha urani kwa kiwango cha juu na vilevile kuwepo Iran katika eneo", nao pia unatokana na uadui mkubwa ilionao Marekani kwa mihimili ya nguvu za Mfumo wa Kiislamu; na akaongezea kwa kusema: "Kuwepo katika eneo ni miongoni mwa nukta za nguvu na usalama wa Iran na mihimili ya kistratejia ya nchi; na hii ndiyo sababu ya upinzani wa maadui."
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi yenye nguvu katika eneo la kistratejia la Magharibi ya Asia na inatekeleza sera zake katika mlingano wa nguvu za kisiasa na kijeshi wa eneo hili pasi na kufuata matakwa ya Marekani. Na hiyo ndiyo sababu ya kuongezeka dhidi yake mashinikizo ya Marekani ikishirikiana na utawala haramu wa Israel na tawala dhalili za Kiarabu. Kutokana na uhusiano wenye maana maalumu, uliopo kati ya wananchi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mashinikizo hayo si tishio kwa mustakabali wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Hakuna shaka yoyote kwamba tajiriba ya ungangari na kusimama imara wananchi wa Iran katika vipindi vigumu zaidi kuliko cha mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa ya hivi sasa ya serikali ya Trump itawapigisha tena mwereka viongozi wa Marekani wanaotaka kubariziana na Mapinduzi ya Kiislamu.../