Zarif: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haistahamili vitisho
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Jamhuri ya Iran kamwe haitastahamili vitisho. Aliyasema hayo jana katika kikao cha pande kadhaa kuhusu makubaliano ya JCPOA huko Nw York, Marekani.
Muhammad Javad Zarif amesema kuwa Iran imekuwa ikikabiliwa na mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi sasa na kwamba tangu wakati huo imeweza kukabiliana na mashinikizo hayo lakini kamwe nchi hii haitavumilia vitisho vyovyote dhidi yake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa taifa la Iran siku zote hutoa jibu kwa vitisho dhidi yake. Zarif amekanusha uwezekano wa kufanya mazungumzo baina ya Iran na Washington na kueleza kuwa: Marekani si nchi ya kuiaminiwa na kufanya nayo mazungumzo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria hatua ya Marekani ya kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuongeza kuwa, Iran haiwezi mara zote kuanza kufanya mazungumzo na Marekani. Amesema kushikamana na makubaliano ya mikataba ni sharti muhimu katika mahusiano ya kimataifa na kwamba Marekani imekuwa ikikiuka mikataba na makubaliano hayo.
Rais Donald Trump wa Marekani tarehe Nane mwezi Mei mwaka huu alichukua uamuzi wa upande mmoja wa kuitoa nchi hiyo katika makubaliano ya JCPOA; hatua iliyolaaniwa na kupingwa pakubwa ndani ya Marekani na katika uga wa kimataifa.