Kuanza upya chokochoko za chinjachinja wa Myanmar dhidi ya Waislamu Warohingya
Kiongozi wa Mabudha wa Myanmar wenye misimamo ya kufurutu mpaka maarufu kama chinjachinja wa Waislamu wa jamii ya Rohingya ameitisha maandamano katika mji wa Yangon ambapo mbali na kuunga mkono jinai zinazofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu Warohingya, ameikosoa vikali pia jamii ya kimataifa kwa kuwafuatilia kisheria makamanda wa jeshi hilo.
Ashin Wirathu, ameanzisha upya kampeni ya kueneza sumu ya chuki dhidi ya Waislamu Warohingya katika hali ambayo hadi mwezi Machi mwaka huu, baraza la watawa wakuu wa Kibudha la Myanmar lilikuwa limempiga marufuku kuhutubia kutokana na kueneza itikadi za kufurutu mpaka katika jamii ya mchanganyiko wa kaumu ya nchi hiyo na kuchochea mauaji ya Waislamu Warohingya katika mkoa wa Rakhine. Kwa hivyo kujitokeza tena Wirathu mbele ya wafuasi wake na kuanzisha tena kampeni za kueneza hisia hasi za kimatapo na chuki za kidini kunazidisha wasiwasi na hofu ndani ya jamii ya Myanmar ya kuanza tena upya mauaji ya Waislamu Warohingya ambayo yamekuwa yakifanywa na wanajeshi wenye chuki na mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka.
Kupigwa marufuku kuhutubia chinjachinja wa Waislamu Warohingya na baraza la watawa wakuu wa Kibudha kunaonyesha kuwa viongozi hao wa kidini wanapinga fikra na itikadi zozote zinazoeneza chuki na hisia hasi za kidini ndani ya jamii ya Myanmar. Kwa sababu Ubudha ni dini inayotetea amani na suluhu na kujiepusha na uenezaji chuki wa aina yoyote ile. Kwa sababu hiyo, matarajio waliyonayo wananchi wa Myanmar ni kuliona baraza hilo la watawa wakuu wa Kibudha linachukua hatua ya kuuelimisha umma sambamba na kuzuia kuanza tena harakati za utendaji jinai zinazochochewa na kuongozwa na Ashin Wirathu. Kuenea fikra na itikadi zake za chuki ndiko kulikowachochea mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka na wanajeshi wenye chuki kuwashambulia Waislamu wa Rohingya mkoani Rakhine, ambapo mbali na kuwaua maelfu miongoni mwao wamewalazimisha wengine zaidi ya milioni moja kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi.
Kwa mujibu wa ripoti za taasisi kadhaa za kimataifa wakiwemo maripota wa Umoja wa Mataifa, askari wa Myanmar wamewabaka kisha wakawatesa na kuwaua wasichana na wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya. Na ndiyo maana katika ripoti yake ya hivi karibuni, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limetaka Jenerali mwandamizi Min Aung Hlaing, ambaye ni mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Myanmar pamoja na makamanda wengine sita wa jeshi hilo wapandishwe kizimbani na kufunguliwa mashtaka.
Wakati huohuo Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu imetangaza kuwa imeshafungua faili la kesi ya watu hao katika chombo hicho cha kimataifa cha sheria. Katika jibu na radiamali aliyotoa kwa tangazo hilo, Ashin Wirathu, chinjachinja wa Waislamu Warohingya amesema, ikiwa mwakilishi yeyote wa mahakama hiyo atatia mguu wake nchini Myanmar kwa lengo la kwenda kuchunguza jinai walizofanyiwa Waislamu Warohingya, siku hiyo yeye ataamua kushika silaha. Sambamba na hayo, kauli ya Jenerali Min Aung Hlaing, kamanda wa jeshi la Myanmar na mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya nchi hiyo kwamba Umoja wa Mataifa au mahakama yoyote ile duniani haina haki ya kuingilia masuala ya ndani ya Myanmar inadhihirisha wasiwasi na hofu aliyonayo, ya yeye na wenzake kufunguliwa kesi katika mahakama ya kimataifa kwa kutenda jinai dhidi ya binadamu.
Tukiiangalia historia ya matukio ya dunia hasa ya hatima za watenda jinai tutabaini kuwa, haijawahi kutokea hata mara moja yeyote kati yao kuukwepa mkono wa sheria na uadilifu. Jinai za kinyama walizofanyiwa Waislamu Warohingya nchini Myanmar ni kubwa na za kutisha, kiasi cha kuzifanya asasi za kimataifa zizitaje kuwa ni jinai dhidi ya binadamu na kusisitizia ulazima wa kupewa adhabu kali kabisa wahusika wa jinai hizo. Kwa hivyo inavyoonyesha, Ashin Wirathu, ambaye yeye mwenyewe ni mmoja wa wahusika wakuu wa uenezaji chuki na kuwahamasisha mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wakawaua Waislamu Warohingya, ana hofu kwamba muda si mrefu yeye pamoja na makamanda watenda jinai wa jeshi la Myanmar watafikishwa mbele ya mahakama za kimataifa au kutokana na mashinikizo ya kimataifa, hatimaye baraza la watawa wakuu wa Kibudha litalazimika kumkabidhi mbele ya vyombo vya sheria. Na ndiyo maana chinjachinja huyo amejitokeza hadharani kupinga kufanyika uchunguzi wowote wa kimataifa kuhusu jinai walizowafanyia Waislamu madhulumu wa jamii ya Rohingya.../