Zarif: Iran inao uwezo wa kuuza mafuta na kulinda uchumi wake
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inao uwezo wa kuuza mafuta yake na pia kulinda vyema uchumi wake.
Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na shirika la habari la Kyodo la Japan na kuongeza kuwa, serikali ya Marekani inaweza kufungua tena njia ya mazungumzo na Iran iwapo tu itarejea kwenye mapatano ya nyuklia iliyojitoa kinyume cha sheria na kuondoa vikwazo vyote ilivyoiwekea Tehran baada ya Trump kutangaza kuitoa Marekani katika mapatano ya JCPOA.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia tabia ya Marekani ya kutoheshimu ahadi zake hata za kisheria na kusisitiza kuwa, inasikitisha kuona kuwa vitendo hivyo vya Marekani vipelelekea kuingia doa hata suala lenyewe la mazungumzo.
Vile vile amesema Tehran inaangalia maslahi yake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuongeza kuwa, Iran inao uwezo wa kuvishinda vikwazo vya Marekani na tayari nchi nyingi duniani zimedharau vikwazo hivyo vipya vilivyotangazwa na Donald Trump na zimetangaza kuwa ziko tayari kushirikiana kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Dk Zarif pia amesema, mbali na nchi tatu za Ulaya za Ujerumani, Uingereza na Ufaransa, nchi nyingine duniani nazo zinayapa umuhimu mkubwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA zikiwemo Russia, China na Japan ambazo zimetangaza bayana kuwa hazishughulishwi na vikwazo vya Marekani na zitaendelea kushirikiana kibiashara na Iran.