Qassemi: Marekani inafadhilisha mikataba ya silaha kuliko haki za binadamu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Marekani inafadhilisha mikataba ya uuzaji silaha kuliko haki za binadamu na hilo ni kinyume cha madai yake ya kutetea haki za binadamu.
Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa kauli hiyo kujibu matamshi ya hivi karibuni ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhusu ugaidi na haki za binadamu nchini Iran. Qassemi amesema: Wakuu wa Marekani sasa wanapima haki za binadamu kwa kutegemea mabadilishano ya kibiashara na dola wanazopokea katika uuzaji silaha." Kwa msingi huo, Qassemi amesema haitegemewi Marekani iwe na msimamo sahihi kuhusu haki za binadamu.
Qassemi ameongeza kuwa, leo wakuu wa Marekani wanaunga mkono baadhi ya tawala zilizo dhidi ya ubinadamu ili ziendelee kuwaangamiza mamilioni ya watoto, wanawake, na watu wasio na hatia katika baadhi ya nchi za eneo. Amesema Marekani inaunga mkono tawala hizo ambazo zimevamia nchi zingine na kusababisha njaa, magonjwa uharibifu wa shule na mahospitali na udondoshaji mabomu katika hafla za harusi na maombolezo kwa kutumia ndege za kisasa kabisa za kivita.
Amesisitza kuwa, katika hali kama hivyo Marekani haina ustahiki wowote wa kuzungumza au kuziamuru nchi zingine kuhusu usalama na haki za binadamu.