Iran yakosoa sera za kiundumakuwili za Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amelaani sera za kigeni za Marekani ambazo msingi wake ni ndoto na kutozingatia uhalisia wa mambo.
Zarif ametoa kauli hiyo kumjibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo ambaye amituhumu Iran kuwa imekiuka azimio la la umoja wa Mataifa ambalo Marekani yenyewe inalikiuka.
Katika ujumbe wa Twitter siku ya Jumapili, Zarif amesema Marekani imekiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hata inatishia nchi ambazo hazitaki kukiuka azimio hilo kwa kutotekeleza vikwazo haramu vya Marekani. Amesema hivi sasa Marekani imegeuka na kiutuhumu Iran eti inakiuka azimio hilo hilo, jambo ambalo linaashiria undumakuwili wa watawala wa Washington.
Mapema, Mike Pompeo, alidai kuwa Iran imefanya jaribio la kombora lenyd uwezo wa kubeba zana za nyuklia kinyume cha azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama.
Kufuatia madai hayo ya Pompeo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Hakuna azimio lolote la Baraza la Umoja wa Mataifa ambalo limepiga marufuku mpango wa makombora wa Iran au kuipiga marufuku kufanya majaribio ya makombora.
Bahram Qassemi ameyasema hayo kujibu madai ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ambaye amedai kuwa, majaribio ya makombora ya Iran yanakiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Qassemi amebainisha kuwa: Mpango wa makombora wa Iran ni wa malengo ya kiulinzi na unatekelezwa kulingana na mahitaji ya nchi.
Azimio 2231 lilipitishwa na Baraza la Usalama kuidhinisha mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA ambayo yalifikiwa Julai mwaka 2015 baina ya Iran na madola sita makubwa duniani, Marekani ikiwemo. Azimio hilo lilitaka Iran iondolewe vikwazo na likapiga marufuku shughuli zozote za silaha za nyuklia. Iran imekuwa ikisisitiza kuwa haina lengo la kuunda silaha za nyuklia. Marekani imekiuka azimio hilo kwa kuiwekea Iran vikwazo.