Mtangazaji wa Press TV anashikiliwa kinyume cha katiba Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50948-mtangazaji_wa_press_tv_anashikiliwa_kinyume_cha_katiba_marekani
Mtaalamu wa masuala ya sheria nchini Marekani amesema kukamatwa na kufungwa gerezani mwandishi habari na mtangazaji wa Televisheni ya Press TV, Bi. Marzieh Hashemi pasina kufahamishwa makosa yake ni kinyume cha katiba ya Marekani.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Jan 18, 2019 00:25 UTC
  • Mtangazaji wa Press TV anashikiliwa kinyume cha katiba Marekani

Mtaalamu wa masuala ya sheria nchini Marekani amesema kukamatwa na kufungwa gerezani mwandishi habari na mtangazaji wa Televisheni ya Press TV, Bi. Marzieh Hashemi pasina kufahamishwa makosa yake ni kinyume cha katiba ya Marekani.

Ricardo J. Bascuas, mhadhiri katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Miami amesema  katiba ya Marekani inapinga kukamatwa raia wa  nchi hiyo bila sababu.

Bi Hashemi, Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika, aliyekuwa akiitwa Melanie Franklin kabla ya kusilimu alitiwa nguvuni Jumapili St. Louis, Missouri na kupelekwa mjini Washington DC ambako amewekwa kizuizini tokea Jumapili bila ya kuelezwa amekamatwa kwa kosa gani.

Mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha IRIB Dkt. Peyman Jebeli amesema,  "Hakuna sababu yoyote ya  kukamatwa Marzieh Hashemi nchini Marekani. Kosa lake kubwa ni kuwa yeye ni mwanamke Mwislamu Mmarekani na tokea mwaka 2003 amekuwa akifanya kazi na Press TV."

Mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha IRIB Dkt. Peyman Jebeli akizungumzia kadhia ya Bi.Marzieh Hashemi

Ameashiria namna wakuu wa Marekani wanavyomdhalilisha Marzieh Hashemi akiwa korokoroni ikiwa ni pamoja na kumvua hijabu yake na kumlazimisha ale nyama ya nguruwe ambayo ni haramu kwa Waislamu na kusema, kitendo hicho ni ukiukwaji wa wazi wa matukufu na thamani za Kiislamu. Aidha amesema mbali na kumnyima chakula cha halali, wakuu wa Marekani pia wamekataa kumpa Bi. Hashemi nguo zinazofaa katika msimu huu wa baridi kali nchini humo.