Dunia yalaani uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51099-dunia_yalaani_uingiliaji_wa_marekani_katika_masuala_ya_ndani_ya_venezuela
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeungana na nchi nyingine duniani kulaani uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 25, 2019 01:09 UTC
  • Dunia yalaani uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeungana na nchi nyingine duniani kulaani uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Tehran inalaani uingiliaji wowote wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Venezuela na inakihesabu kitendo chochote kilicho kinyume cha katiba kuwa ni sawa na mapinduzi dhidi ya wananchi, serikali na taifa hilo zima la Amerika ya Latini.

Wakati huo huo, Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia naye amelaani uingiliaji wa Marekani na nchi za Magharibi katika masuala ya ndani ya Venezuela na kusema kuwa lengo la madola hayo ajinabi ni kuzusha vujo na machafuko nchini humo.

Nchi nyingine mbalimbali duniani zinaendelea kulaani uingiliaji wa masuala ya ndani ya Venezuela unaofanywa na madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani.

 

Rais Maduro wa Venezuela amewataka wananchi wa nchi hiyo wawe macho na wachukue tahadhari kubwa katika kipindi hiki kigumu ambacho nchi hiyo inapambana na njama za kila upande hasa kutoka kwa Marekani.

Mgogoro mpya umezuka nchini Venezuela baada ya Juan Guaido, spika wa bunge aliyefutwa kazi, kujitangazia urais wa nchi hiyo. Marekani ilikuwa nchi ya kwanza kabisa kumtambua rasmi Guaido licha ya kwamba ni kiongozi wa waasi ambaye amekwenda kinyume kabisa na katiba ya Venezuela. 

Nchi kama Brazil zimetangaza wazi kuwa zitaendelea kuiunga mkono serikali halali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Nicolás Maduro na ambayo imechaguliwa kidemokrasia nchini Venezuela.