Rais Rouhani: Umoja, dawa mjarabu ya kuzima ugaidi
-
Ras Rouhani na mwenzake wa Serbia
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuenea jinai na ugaidi ni katika changamoto kuu zinaolikabili eneola Mashariki ya Kati na dunia nzima kwa ujumla na hivyo kuna haja ya watu wa dini mbali mbali kushirikiana kwa lengo la kukabiliana na matatizo hayo.
Katika mkutano na mwenzake wa Serbia, Tomislav Nikolic hapa mjini Tehran, Rais Hassan Rouhani amekosoa jitihada zinazofanywa na baadhi ya madola ya kibeberu ya kuuoanisha ugaidi na dini tukufu za Mwenyezi Mungu. Rais wa Iran ameongeza kuwa, dini takatifu za Mbinguni na haswa Uislamu, zinaunga mkono umuhimu wa udugu, watu wa jamii zote kuamiliana kwa wema na kupinga harakati za ugaidi.
Wakati huo huo, Rais Hassan Rouhani amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano kati ya Iran na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na nchi za Balkan. Rais wa Iran amesema: "Tehran na Belgrade zina uwezo na nafasi nzuri ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyuga tofauti."
Kwa upande wake, Rais wa Serbia Tomislav Nikolic amesema nchi yake iko tayari kuimarisha uhusiano na Tehran na kusisitiza kuwa, mafanikio ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na Kundi la 5+1 yanaashiria izza ya Jamhuri ya Kiislamu.
Nikolic ambaye aliwasili Tehran jana Jumamosi, alitazamiwa kushiriki ufunguzi wa Mkutano wa 5 wa Kimataifa wa Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu, ulioanza leo Jumapili hadi tarehe 22 ya mwezi huu wa Aprili.