Iran yaionya Saudi Arabia kutokana na chokochoko zake dhidi ya Tehran
Msaidizi maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) katika masuala ya kimataifa ameionya Saudi Arabia iache kushirikiana na Marekani katika chokochoko zake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Hossein Amir-Abdollahian ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Iwapo watawala wa Saudia hawatoacha kushirikiana na kuwa vibaraka wa Marekani katika vita vya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, basi wasubiri maamuzi mapya na ya kushtua ya Tehran."
Amesisitiza kuwa, muda wa kuendelea siasa chafu za Saudi Arabia, Imarati na Israel unaisha kwa kasi sana.
Siku ya Alkhamisi, Saudia iliitisha kikao cha viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kingine cha viongozi wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi mjini Makka na siku ya Ijumaa ikaitisha kikao cha viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC huko huko Makka.
Vikao hivyo vyote viliitishwa ili kuyatumikia madola ajinabi ya kibeberu lakini vilizidi kuonesha kuchanganyikiwa utawala wa ukoo wa Aal Saud baada ya kuzuka mzozo na hitilafu kubwa kati ya washiriki wa vikao hivyo hususan baina ya Qatar na kundi lililoiwekea vikwazo nchi hiyo yaani Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain.