Jun 05, 2019 08:20 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Muamala wa Karne kamwe hautofikia malengo yake

Kiingozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kusisitiza kwamba mpango unaoitwa 'Muamala wa Karne' hautofikia malengo yake, amepongeza nchi za Kiarabu na kadhalika makundi ya Palestina yaliyopinga mpango huo.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo katika hotuba za swala ya Idil-Fitri iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran katika eneo la Musalla wa Imam Khomeini (MA) ambapo sambamba na kutoa pongezi kwa umma wa Kiislamu na wananchi wa Iran kwa mnasaba wa Idi hii kubwa amesema kuwa suala la Palestina na njama za uhaini za Marekani kupitia mpango wake wa 'Muamala wa Karne' ni kadhia ya kwanza kwa ulimwengu wa Kiislamu. Amesema kuwa baadhi ya nchi za Kiislamu kama vile Bahrain na Saudi Arabia zimefanya hiana kutokana na kuhusika na uandaaji wa mpango huo mchafu. Kiongozi Muadhamu ameashiria uenyeji wa Bahrain kwa mkutano wa kiuchumi wa mpango wa Muamala wa Karne na kusema kuwa mkutano huo uliitishwa na Wamarekani, lakini viongozi wa Manama kwa udhaifu na kutokana na roho mbaya dhidi wananchi na dhidi ya Uislamu wamekubali kuwa wenyeji wake. Amesisitiza kwamba watawala wa Bahrain na Saudia lazima wafahamu kwamba, mienendo yao hiyo itaishia kukwama katika kinamasi.

Ibada ya Swala ya Idil-Fitri iliyoswaliwa leo mjini Tehran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewashukuru pia raia wa Iran kutokana na kushiriki kwao kwa wingi katika matembezi ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kuongeza kwamba, ushiriki huo mkubwa na imara wa wananchi katika harakati hiyo, umekuwa na taathira katika siasa za dunia na kuwakatisha tamaa maadui wa taifa la Iran sambamba na kutia dosari mahesabu yao. Ayatullah Ali Khamenei ameashiria pia baadhi ya ada nzuri  na za kuvutia za Kiislamu ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani likiwemo suala la kusaidiana ambalo limestawi nchini hapa, na kusifu ushiriki wa wananchi kwa ajili ya kusaidia kutoa futari katika misikiti, husseiniya na maeneo ya kijamii, kama ambavyo pia ametaka kusaidiwa waathirika wa mafuriko ya hivi karibuni nchini. Ibada ya swala ya Idil Fitri mjini Tehran imeongozwa na Kiongozi Muadhamu. Waislamu wa Iran asubuhi ya leo wameshiriki ibada hiyo katika maeneo yote ya nchi hii baada ya kumalizika mwezi Mtukufuu wa Ramadhani. Nchi nyingi za Kiislamu ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeswali swala ya Idil-Fitri  leo Jumatano.

Tags