Jun 24, 2019 12:52 UTC
  • Zarif: Vikwazo vya Marekani vinalemaza vita dhidi ya mihadarati

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na ugaidi wa kiuchumi wa nchi hiyo ya kibeberu dhidi ya taifa la Iran umekuwa kizingiti kikubwa katika ushirikiano wa kimataifa hususan katika vita dhidi ya mihadarati.

Muhammad Javad Zarif amesema hayo leo Jumatatu katika kongamano lililofanyika hapa mjini Tehran kwa mnasaba wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Magendo ya Mihadarati na Matumizi ya Dawa Haramu za Kulevya.

Dakta Zarif ameeleza bayana kuwa, Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zinapaswa kubebea dhima ya matokeo mabaya ya kulemaa vita dhidi ya mihadarati.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amenukuu takwimu za Umoja wa Mataifa zinazoonesha kuwa, Iran ndiye mbeba bendera wa vita dhidi ya dawa za kulevya duniani.

Dakta Zarif akihutubia kongamano la vita dhidi ya mihadarati mjini Tehran

Kwa mujibu wa takwimu za UN, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka jana iliweza kunasa asilimia 80 ya afiuni yote duniani, sawa na tani 800 za mihadarati hiyo.

Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, Iran imefanikiwa kunasa tani 12 elfu za aina mbalimbali ya mihadarati.

Aidha Iran imekuwa mhanga mkubwa wa ulanguzi wa mihadarati duniani, kwani maafisa usalama wake 8,800 wameuawa shahidi katika vita dhidi ya mihadarati huku wengine 12,000 wakijeruhiwa.

Mwaka 2000 na 2001, ukulima wa mihadarati Afghanistan ulikuwa ni tani 200 lakini baada ya askari wa Marekani kuvamia nchi hiyo, kiwango hicho kimeongezeka na kufika tani 10,000

 

Tags