Sheikh Isa Qassim: Trump anataka kuiuza Palestina na matukufu yake
Mwanazuoni maarufu wa Kiislamu nchini Bahrain, Sheikh Isa Qassim sambamba na kulaani hatua ya utawala wa Manama kuwa mwenyeji wa Kongamano la Kibiashara linalotazamiwa kuanza leo nchini humo kwa shabaha ya kuzindua mpango wa 'Muamala wa Karne' amesema mpango huo wa Rais Donald Trump wa Marekani unakusudia kuwapokonya Wapalestina haki zao zote na kuuza kila kitu kinachomilikiwa nao yakiwemo maeneo matakatifu.
Sheikh Isa Qassim ameyasema hayo katika Mkutano wa Muqawama wa Vijana katika mji mtakatifu wa Qum, kusini mwa Tehran hapa nchini Iran usiku wa kuamkia leo ambapo amebainisha kuwa, ulimwengu wa Kiislamu hauna changuo jingine ghairi ya kuukataa katakata mpango huo wa 'Muamala wa Karne'.
Mwanachuoni huyo wa Bahrain amesisitiza kuwa, kuukataa mpango huo wa Marekani na Wazayuni dhidi ya Wapalestina ni kukataa utumwa na kukukumbatia uhuru.
Ayatullah Sheikh Issa Qassim amesema kitendo cha kuwakaribisha nchini Bahrain Wazayuni ni hatua moja kuelekea katika njia ya kujidhalilisha kwa adui mkubwa zaidi kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Mwanachuoni huyo maarufu wa Kiislamu nchini Bahrain amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ndiye adui nambari moja wa ulmwengu wa Kiislamu ambaye hapaswi kukaribishwa, kupokewa wala kupewa mkono.
Sheikh Isa Qassim anahudhuria Mkutano wa Pili wa Muqawama wa Vijana mjini Qum, ambao umewaleta pamoja vijana kutoka nchi 60 duniani ambao wamekumbuka na kuwaenzi vijana waliouawa shahidi wakipambana na udikteta wa utawala wa Aal-Khalifa nchini Bahrain.