Jul 05, 2019 07:24 UTC
  • Zarif: Hatua ya Iran kupunguza ahadi ilizojifunga nazo itazuia JCPOA kuvunjika kikamilifu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria ukiukaji ahadi wa madola ya Ulaya katika kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya Iran na kueleza bayana kwamba, hatua ya kupunguza ahadi ilizojifunga nazo Iran kwa mujibu wa mapatano hayo inachukuliwa kwa shabaha ya kuzuia JCPOA isivunjike kikamilifu.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika mahojiano yalichopishwa jana Alkhamisi na gazeti la New York Times la Marekani na kuongeza kuwa, hatua za hivi karibuni za Iran za kupunguza kiwango cha uwajibikaji wake kwenye JCPOA zinakusudia kuyaokoa makubaliano hayo yasiporomoke, kwani kusambaratika kwake kutakuwa kwa madhara ya pande zote husika.

Amefafanua kuwa, endapo madola ya Ulaya yatachukua hatua za lazima kwa ajili ya kutekeleza ahadi na wajibu wao kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA, basi Tehran inaweza kuangalia upya hatua ilizozichukua, vinginevyo Iran itaendelea kupunguza uwajibikaji wake kwenye mapatano hayo kwa mujibu wa kifungo cha 36 cha JCPOA. 

Dakta Zarif amebainisha kuwa, "JCPOA inasalia kuwa makubaliano bora zaidi kwa kadhia hii ya nyuklia ya Iran, na Tehran itaendelea kufungamana na mapatano hayo madhali pande zilizosalia kwayo (Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Russia na China) nazo zitatekeleza wajibu wao.

EU imekuwa ikisuasua kutekeleza mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati ya Iran na Umoja wa Ulaya (INSTEX)

Iran imevuka kiwango cha kilo 300 za akiba ya urani iliyorutubishwa kilichoainishwa katika makubaliano ya JCPOA na kusisitiza kuwa, iwapo pande nyingine za makubaliano hayo zitatekeleza majukumu yao, Tehran nayo itarejea katika kiwango kilichoainishwa. 

Ifahamike kuwa, uamuzi wa Iran wa kuongeza akiba ya urani umefanyika kwa mujibu wa vipengee vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na wala hatua hiyo haihesabiwi kwamba ni ukiukaji wa makubaliano yenyewe. 

Tags