Jul 14, 2019 06:37 UTC
  • Zarif: Liwe liwalo, Iran itaendelea kuuza mafuta yake nje

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria vikwazo haramu vya Marekani dhidi ya taifa hili na kusisitiza kuwa, Tehran itaendelea kuyauza mafuta yake nje ya nchi bila kubabaishwa na chochote.

Mohammad Javad Zarif aliyasema hayo jana jioni katika mazungumzo yake ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Jeremy Hunt ambapo ameitaka serikali ya London iharakishe mchakato wa kuiachia meli ya mafuta ya Iran inayoizuilia Jabal Tariq.

Dakta Zarif ameeleza bayana kuwa, ilitarajiwa kuwa Uingereza ingeendelea kupuuza vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hili, kwa shabaha ya kuyanusuru mapatano ya nyuklia ya JCPOA, lakini Tehran imeshangazwa na hatua ya London ya kuisimamisha na kuiuzulia meli yake ya mafuta. 

Itakumbukwa kuwa jeshi la majini la Uingereza tarehe 5 mwezi huu wa Julai lilisimamisha na kushikilia meli ya mafuta ya Iran katika Lango Bahari la Jabal Tariq (Gibraltar) kwa kisingizio kwamba, imekiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria.

Meli ya mafuta ya Iran ya Grace 1 inayoshikiliwa na Uingereza

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekadhibisha madai hayo ya Uingereza na kuitaka London iiachie mara moja meli hiyo ili iendelee na safari yake.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amesema Iran ina haki ya kuendelea kuuza mafuta yake nje ya nchi, lakini serikali ya London inatiwa wasiwasi na kuendelea kuongezeka taharuki katika Ghuba ya Uajemi.

Tags