Rais wa Ufaransa akabidhiwa jukumu la kufikisha ujumbe wa G7 kwa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55595-rais_wa_ufaransa_akabidhiwa_jukumu_la_kufikisha_ujumbe_wa_g7_kwa_iran
Kundi la G7 linaloundwa na madola saba makubwa ya viwanda duniani limemkabidhi Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa jukumu la kufikisha ujumbe na kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 25, 2019 08:31 UTC
  • Rais wa Ufaransa akabidhiwa jukumu la kufikisha ujumbe wa G7 kwa Iran

Kundi la G7 linaloundwa na madola saba makubwa ya viwanda duniani limemkabidhi Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa jukumu la kufikisha ujumbe na kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Shirika la habari la Ufaransa limeinukuu duru moja katika ofisi ya rais wa Ufaransa na kuripoti kuwa, baada ya mazungumzo na majadiliano waliyofanya juu ya suala hilo jana usiku kusini magharibi mwa Ufaransa, viongozi wa kundi la G7 wamekubaliana kuwa rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron afanye mazungumzo na kufikisha ujumbe kwa Tehran kwa niaba yao.

Duru hiyo aidha imedai kwamba, kipaumbele cha madola hayo kingali ni cha kuizuia Iran isimiliki silaha za nyuklia na kuondoa hali ya wasiwasi na mivutano katika Ghuba ya Uajemi.

Kikao cha 45 cha viongozi wa nchi saba kubwa za viwanda duniani G7 ambazo ni Marekani, Uingereza, Ujerumani, Italia, Canada, Ufaransa na Japan kilianza jana katika mji wa Biarritz kusini magharibi mwa Ufaransa.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa (kulia) akizungumza na Waziri Zarif mjini Paris

Itakumbukwa kuwa mnamo siku ya Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif alikutana na kufanya mazungumzo mjini Paris na viongozi wa Ufaransa akiwemo rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron. Katika na baada ya mazungumzo hayo, Zarif alisisitiza kwamba, Umoja wa Ulaya unapaswa kutekeleza ahadi na majukumu yake kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na vile vile ahadi ulizotoa baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.

Baada ya Marekani kujiondoa kinyume cha sheria katika JCPOA mwezi Mei mwaka uliopita wa 2018, Ujerumani, Uingereza na Ufaransa ziliahidi kuwa, zitadhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran ili kuyalinda makubaliano hayo. Hata hivyo licha ya kukabiliana kwa maneno na kisiasa na hatua za Marekani, nchi hizo tatu hadi sasa hazijachukua hatua yoyote kivitendo ya kutekeleza ahadi  zilizotoa kwa ajili ya kuyalinda makubaliano hayo ya nyuklia.../