Sep 27, 2019 12:37 UTC
  • Sheikh Siddiqi: Kujihami kutakatifu taifa la Iran kumeacha athari katika historia ya leo

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, miaka minane ya kujihami kutakatifu taifa la Iran mbele ya uchokozi wa utawala wa dikteta Saddam wa Iraq kumeacha athari katika historia ya leo.

Hujjatul Islam wal Muslimin Sheikh Kadhim Siddiqi amesema hayo mbele ya hadhara kubwa ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa hapa Tehran ambapo sambamba na kuashiria kumbukumbu ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu ameeleza kuwa, baada ya tukio la Karbala hakuna tukio lililokuwa na taathira katika historia kama tukio la kusimama kidete na kujihami kutakatifu taifa la Iran mbele ya uvamizi na vita vya kichokozi vya utawala wa dikteta Saddam Hussein.

Sheikh Kadhim Siddiqi amesema, wakati wa vita hivyo madola yote ya dunia yalikuwa yakimuunga mkono adui mvamizi, jeshi la Iran lilikuwa limesambaratika, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH halikuwa na tajiriba ya kutosha ya vita, hata hivyo wananchi wa Iran wakifuata miongozo ya Imam Khomeini MA walisimama kidete kwa miaka minane dhidi ya madola makubwa ulimwenguni.

Wiki ya Kujihami Kutakatifu

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran amekosoa pia undumakuwili katika suala zima la haki za binadamu na kueleza kwamba, kuna haja ya kupatiwa ufumbuzi matatizo ya Waislamu wa Kashmir, Mashia wa Nigeria, Waislamu wa Kishia Bahrain pamoja na Waislamu wa Kishia huko Saudi Arabia ambao haki zao zinakanyagwa na kwamba, nchi zote za Kiislamu zinapaswa kufanya juhudi katika hilo.

Tags