Jun 14, 2024 11:28 UTC
  • Ayatullah Khatami: Mirengo yote ina wagombea wao kwenye uchaguzi ujao wa Rais nchini Iran

Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya hapa Tehran amesema kuwa, hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeimarika mno kiasi kwamba mirengo yote ina wawakilishi wao katika uchaguzi ujao wa Rais humu nchini.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo kwenye khutba za leo za Salama ya Ijumaa ya hapa Tehran na huku akigusia siku na mikesha hii mitakatifu ya msimu wa Hija amesema kwamba Arafa ni siku ya nuru na Alhamdulillah, miaka yote wananchi Waislamu wa Iran hujitokeza kwa wingi kwenye dua ya pamoja ya Arafa.

Amma kuhusiana na jinai za utawala wa Kizayuni huko Palestina, Imam wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amesema kwamba, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, matukio ya Ghaza na kuuliwa kwa umati karibu watu 40,000 wengi wake wakiwa ni wanawake na watoto, kunaliza na kunaumiza mno nyoyo. Taifa la Iran linahuzunika kwa jinai hizo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitosita hata kidogo kuwa pamoja na wananchi madhlumu wa Ghaza.

Amma kuhusu uchaguzi wa wiki ijayo wa Rais wa Iran, Ayatullah Khatami amesema kuwa, kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi huo kutazidi kukamilisha hamasa waliyoonesha wakati wa maziko ya mashahidi Rais Ebrahim Raisi, Amir-Abdollahian na wenzao.

Tags