Rais Rouhani akiwa Japan: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran havimnufaishi yoyote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58009-rais_rouhani_akiwa_japan_vikwazo_vya_marekani_dhidi_ya_iran_havimnufaishi_yoyote
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujiondoa kinyume cha sheria kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA haina maslahi kwa Marekani yenyewe wala upande wowote wa mapatano hayo ya kimataifa.
(last modified 2026-05-13T18:57:29+00:00 )
Dec 20, 2019 23:35 UTC
  • Rais Rouhani akiwa Japan: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran havimnufaishi yoyote

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujiondoa kinyume cha sheria kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA haina maslahi kwa Marekani yenyewe wala upande wowote wa mapatano hayo ya kimataifa.

Rais Rouhani amesema hayo katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe jijini Tokyo na kueleza bayana kuwa, "Nchi zote zina wajibu wa kuheshimu Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu JCPOA. Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni aina fulani ya ugaidi wa kiuchumi, na nchi zote zinazopambana na ugaidi zinapaswa kupinga vikwazo hivyo kwa kauli moja."

Dakta Rouhani amesema makubaliano hayo ya nyuklia ya Iran ni muhimu mno kwa pande zote, na kitendo cha Marekani kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa hakikuwa cha kimantiki.

Rais Rouhani akipokewa na Waziri Mkuu wa Japan jijini Tokyo

Rais wa Iran ameashiria kuhusu hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya kupunguza uwajibikaji wake kwenye makubaliano hayo hatua kwa hatua na kusema kuwa, "Ulaya imeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa vipengee vya makubaliano hayo. Nchi za Ulaya zinapaswa kutekeleza wajibu wao ipasavyo."

Amesema: Tunamai Japan na nchi nyingine za dunia zitafanya jitihada za kuyabakisha hai mapatano hayo ya JCPOA. Rais Rouhani amesema Iran itaendeleza juhudii zake za kuhakikisha amani na usalama vinatawala sio tu katika eneo la Asia Magharibi bali kote duniani kwa ujumla na kuongeza kuwa, Tehran itaendelea kuwa na ushirikiano wa udugu na nchi za eneo na majirani zake.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe amesema nchi yake ina hamu ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga mbalimbali. Amesema, "Mikutano na mazungumzo baina ya maafisa wa serikali za nchi mbili hizi katika miaka ya hivi karibu yamechangia katika kuimarika uhusiano wa Tehran na Tokyo."

Rais Rouhani na Shinzo Abe wakiongoza jumbe zao katika mazungumzo jijini Tokyo

Amesema Japan ingependa kuona hali ya taharuki katika eneo la Asia Magharibi inapungua sambamba na kupatikana uthabiti katika eneo hilo la kistratajia.

Waziri Mkuu wa Japan ameongeza kuwa, "Ninatumai Iran itaendelea kufungamana na JCPOA licha ya Marekani kujiondoa kwenye makubaliano hayo, kwa maslahi ya amani na uthabiti wa eneo.