Rouhani: Wananchi ni chanzo halisi cha nguvu na uwezo wa Iran
Rais Hassan Rouhani amesema wananchi wa Iran ndio chimbuko la kweli na halisi la nguvu na uwezo mkubwa wa taifa hili.
Rais Rouhani amesema hayo mapema leo katika kikao cha Baraza la Mawaziri hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, "hakuna uwezo unaoshinda ushiriki wa watu, muqawama, umoja na moyo wao wa kujitolea."
Amesema kuwashirikisha wananchi wa Iran katika masuala mbalimbali, umoja na mshikamano wao ni nguzo muhimu ambazo Iran imekuwa ikizitegemea katika nyakati zote za misukosuko na matatizo.
Rais wa Iran amesema maadui wa taifa hili hawaogopi uwezo wa kijeshi, kiulinzi na kiuchumi wa Iran, bali kinachowatisha zaidi ni uwezo wa kuitamaduni wa taifa la Iran.
Kadhalika Dakta Rouhani ameashiria kuhusu umuhimu wa wananchi wa Iran kushiriki kwa wingi katika uchaguzi ujao wa Bunge. Uchaguzi huo pamoja na ule wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchangua Kiongozi Muadhamu unatazamiwa kufanyika Februari 21.
Rais wa Iran ameeleza bayana kuwa, "ni muhimu kwa wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi, vinginevyo tunakuwa na uchaguzi kama chaguzi zinazoshuhudiwa katika nchi fulani za Ulaya, ambapo ushiriki wa watu huwa wa asilimia 15 hadi 20."